Saturday, February 11, 2012

MADAKTARI WAREJEA



HUDUMA za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (MOI) jana zilirejea katika hali yake ya kawaida baada ya madaktari waliokuwa kwenye mgomo, kurudi kazini huku makundi ya wanaharakati yakiongeza shinikizo la kung’olewa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya.

Madaktari hao wamerejea kazini baada ya mgomo huo  uliochukua siku 17 kushinikiza Serikali itekeleze madai yao kadhaa, likiwamo suala la nyongeza ya posho na kuwajibishwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutekelezwa.
Mgomo huo ulimalizika juzi baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukutana na madaktari hao jijini Dar es Salaam na kuahidi kutekeleza baadhi ya madai yao, huku akiwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
Hatua hiyo ya Serikali ilitokana na tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwa watendaji hao, ikiwamo kashfa ya kudaiwa kuingiza nchini robo tatu ya vifaa bandia vya vipimo vya Ukimwi kutoka Korea Kusini, kuanzisha kampuni ya kusambaza nguo kwa madaktari na wauguzi na kuiingiza kinyemela kampuni inayofanya usafi ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.


Jana Ofisa Habari Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aliegaesha alilithibitishia gazeti hili kuwa huduma katika hospitali hiyo, zimerejea katika hali ya kawaida ingawa idadi ya wagonjwa waliojitokeza, bado ni ndogo ikilinganishwa na siku za nyuma.
“Madaktari wa JWTZ wameondoka leo (jana), hii ni kutokana na kurejea kwa madaktari wote waliokuwa kwenye mgomo kutokana na mkutano wa maridhiano uliofanyika jana (juzi) baina yao na Waziri Mkuu,” alisema Aliegaesha.
Msemaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Frank Matua, naye alisema huduma katika taasisi hiyo zimerejea katika hali ya kawaida kwa vitengo vyote, zikiwamo za  kliniki.
“Huduma zinapatikana sasa. Kliniki zote zilizofungwa wakati wa mgomo sasa zimefunguliwa. Changamoto ni kwamba idadi ya wagonjwa waliofika leo (jana) kupata huduma ni bado ndogo,” alisema Matua na kuongeza;
“Hili linaweza kuwa limesababishwa na wao kutokuwa na taarifa za uhakika kuhusu kumalizika kwa mgomo huo.”
Awali madaktari hao waligoma wakidai kupatiwa nyumba za kuishi, kukopeshwa magari, kupatiwa bima ya matibabu, kulipwa fedha kwa ajili ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi na magumu na kuboreshewa mazingira ya kazi hospitalini, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa vingine muhimu.

Huduma mikoani

Mbali ya Muhimbili na MOI , huduma hizo pia  zimeanza kurejea katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Mbeya na Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.
Madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma walitangaza juzi jioni kuwa wamesitisha mgomo na sasa wanarejea kazini kama kawaida.
Katibu wa Afya wa Hospitali hiyo, Isack Kaneno alithibitisha kupewa taarifa ya madaktari kusitisha mgomo na kueleza kuwa huduma sasa zitaendelea kama kawaida.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, hali imetengemaa baada ya madaktari waliokuwa wamegoma kurudi kazini jana.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando, Dk Charles Majinge, alisema mwitikio wa madaktari kurudi kazini ni mzuri ingawa bado utawala wa hospitali hiyo hadi jana mchana ulikuwa unafanya tathmini ya idadi ya waliorejea.


Ombi kwa Rais Kikwete
Katika hatua nyingine, baadhi ya madaktari waliorejea kazini, wamemtaka Rais Kikwete awafukuze Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya.

Dk Godfrey Kimaria, alisema kutokana na maelezo ya Waziri Mkuu, mawaziri hao hawana budi kufukuzwa kwa kuwa wamesababisha maafa.Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Edwin Chitage, alisema  kilichofanywa na madaktari ni mapinduzi makubwa kutokana na umoja waliouonyesha na Serikali inatakiwa kuisafisha wizara hiyo ili kuleta mwonekano sahihi wa kiutendaji.

Shinikizo zaidi kwa Mponda, Nkya
Siku moja baada ya Serikali kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali Dk Mtasiwa, wanaharakati nchini, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete, kumng'oa  Waziri wa Afya na Naibu wake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wanaharakati wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Jukwaa la Katiba na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), walisema, Dk Mponda na Dk Nkya wanapaswa kuwajibika kwa madhara yaliyotokana na mgomo huo.

Mkurugenzi wa LHRC, Helen Kijo Bisimba alisisitiza kuwa ni lazima Rais Kikwete awawajibishe mawaziri hao kama watashindwa kujiuzulu kwenye nafasi zao.

 “Nawaomba viongozi hawa wajiuzulu haraka ili uchunguzi uweze kufanyika. Wasimsubiri Rais awawajibishe, waonyeshe uzalendo wao kwa Watanzania wa kufanya uamuzi bila kushurutishwa,” alisema.

Bisimba aliupongeza uamuzi wa madaktari kurejea kazini akisema ni uamuzi wa kiungwana uliolenga kuokoa maisha ya Watanzania lakini Serikali nayo itimize ahadi zake kwao, alisema

Rais wa CWT, Gratian Mukoba naye alisema chama hicho kingependa kuona Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na Naibu wake,wanajiuzulu kwa kuwa wamesababisha maafa makubwa Muhimbili.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangira alisema wameamua kurudi kazini kuitikia wito wa makundi mbalimbali ya kijamii. Aliongeza kuwa itakapofika Machi 3, mwaka huu, watakaa na kamati yao kutathmini matokeo ya mazungumzo yao na Serikali.


Viongozi wa  Dini
Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhaji Musa Salum amesema Serikali inapaswa kupongezwa kwa hatua iliyofikia ya kuwarudisha madaktari kazini.

Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Kagera, Dk Methodius Kilaini, amelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata wanaharakati wa haki za binadamu huku akiitaka Serikali kuwasikiliza kwani wanatetea haki za Watanzania.


Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jana Askofu Kilaini alisema polisi haikupaswa kuwakamata wanaharakati hao kwani wapo kwa lengo la kutetea haki za Watanzania.

Mbunge wa Jimbo Ubungo John Mnyika amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa Waziri Mponda na Naibu wake Dk Lucy Nkya haraka ili kupisha uchunguzi baada ya kuonyesha udhaifu wa kutatua mgogoro wa madaktari 

na Serikali.








                  WAZIRI WA AFYA BADO ANATAFAKARI 




WAKATI Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa wakisimamishwa kazi, Waziri wa wizara hiyo, Dk Haji Mponda, amesema kukimbilia kujiuzulu kabla ya kutathimini jambo husika siyo suluhu ya kutatua tatizo.

Dk Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya, wamekuwa wakishinikizwa na madaktari pamoja na mawaziri wenzao, kuwajibika kwa kujiuzulu kutokana na mgomo huo wa zaidi ya wiki mbili uliotikisa nchi.Akizungumza jana na gazeti hili kwa njia ya simu lililotaka kujua msimamo wake, kama yuko tayari kuwajibika kutokana na mgomo huo, ama la Dk Mponda  alisema;


"Kukimbilia kujiuzulu siyo suluhu sana ya tatizo. Kwasababu kama ni hivyo, watu wanaweza kuharibu mambo kwa maksudi wakitegemea watajiuzulu na kukaa pembeni."


Alieleza kwamba hadi jana jioni,  hakuwa na uamuzi wowote kuhusu hilo na alikuwa akiendelea na majukumu yake kama kawaida huku akisisitiza;  


"Unajua mtu anaweza kufikiria zaidi kujiuzulu  kama atakuwa amefanya au amesababisha kitu na yeye mwenyewe nafsi yake ikathibitisha hilo. "


Alisema binafsi, ameguswa na mgomo huo wa madaktari ambao umeathiri huduma za afya nchini, huku baadhi ya watu wakipata madhara zaidi ya maradhi.


Lakini, alipoulizwa kwamba kutokana na hali hiyo, haoni kwamba alipaswa kuwajibika kwa kujiuzulu kama sehemu ya kuumizwa na madhara yaliyowapata Watanzania kutokana na Wizara yake  alijibu; "Naomba ni reserve(nihifadhi) kauli yangu katika hilo. Lakini, nani wanataka nijiuzulu, ni wewe (mwandishi) au nani? Maana sijasikia hilo unalosema. Nikisikia nitaamua."     

 
Alifafanua kwamba kuwajibika wakati mwingine baadhi ya watu wamekuwa wakitafsiri dhana hiyo tofauti .

"Kwa mfano, mimi nimeguswa sana na mgomo wa madaktari, nawapenda sana Watanzania, sasa hapo kuna tofauti kidogo."


Dk Mponda alisema ndiyo maana alikuwa akifanya jitihada zote kuhakikisha anakutana na madaktari hao kuhakikisha mgomo huo unamalizika, lakini bahati mbaya juhudi hizo hazikufanikiwa haraka.


"Kwakweli nimeguswa sana na mgomo huo wa madaktari, ndiyo maana nimekuwa  nikifanya kila jitihada kuhakikisha unamalizika, lakini bahati mbaya hilo halikutokea. Kwa hiyo, nimeumia sana," alisisitiza  Dk Mponda, baada ya  kuulizwa tena kwamba kama ameguswa ni kwanini  asiwabijike kwa kujiuzulu hata kama hakutenda kosa.


Alisema anatambua umuhimu na dhana ya uwajibikaji, lakini akasisitiza kuwa "Siwezi kusema zaidi kwa sasa. Wakati ukifika nitaweza kuzungumza."



Mawaziri wenzake

Katika kikao cha kazi kilichofanyika Jumanne iliyopita chini ya Waziri Mkuu Pinda, ilidaiwa kutoka ndani ya kikao kwamba baadhi ya mawaziri  walimweleza mkuu huyo wa shughuli za Serikali bungeni kwamba, Waziri wa Afya na Naibu wake, walipaswa kujiuzulu.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa suala la mgomo huo, lisingeweza kushughulikiwa kimyakimya, na kwamba ilikuwa lazima Serikali kukubali kukaa na madaktari hao na kusikiliza malalamiko yao.


Tayari, pendekezo hilo lilishatolewa na Kamati ya Wabunge wa CCM, ambao walitaka Dk Mponda, Naibu wake Dk Nkya na Katibu Mkuu Nyoni wajiuzulu na wakikataa wawajibishwe.







HOFU YA WAPINZANI KUCHUKUA NCHI YAZIZIMA, WABUNGE WAKE WAPINGA MABADILIKO YA KATIBA NDANI YA CHAMA

 MSUGUANO mpya umeibuka ndani ya (CCM) baada ya Kamati ya Wabunge wa CCM kupinga mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ya chama hicho yanayowaondoa kuwania nafasi za chama, huku wakihoji uongozi ulikopata mamlaka ya kufanya marekebisho hayo bila kuwashirikisha.

Suala la mabadiliko hayo ni miongoni mwa mambo yaliyotarajiwa kuibuka katika mkutano wa wabunge hao na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambao ulitarajiwa kufanyika jana usiku kwenye ukumbi wa mikutano wa chama hicho uliopo makao makuu, Dodoma.

Mkutano huo wa Rais Kikwete na wabunge wa chama chake, unatangulia vikao vya juu vya chama hicho, ambavyo ni Kamati Kuu ya CCM (CC) inayotarajiwa kukutana leo na ukifuatiwa na Halmashauri Kuu (NEC) kesho, ili kubariki mabadiliko hayo ya Katiba ya CCM.

Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika juzi usiku, zinasema wabunge hao walisema marekebisho hayo yamefanyika bila kuwashirikisha, hali inayowatia wasiwasi kwamba huenda CCM kikapoteza uongozi wa nchi.

Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho zinasema, hofu kubwa waliyonayo wabunge ni mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kufanywa katika katiba kwamba huenda yakabadili mfumo wa uchaguzi wa ngazi zote ndani wa CCM, huku wao wakiathirika kwa kiasi kikubwa.
Mchakato wa marekebisho hayo umekuwa ukifanywa na Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya CCM chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa na matokeo ya kazi yake yatawasilishwa katika vikao vya CC leo na NEC kesho.


Miongoni mwa mabadiliko ambayo yamekuwa yakitajwa ni pamoja na wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuzuiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama, ikiwa ni hatua ya kufanya mageuzi yenye lengo la kuondoa tatizo la baadhi ya watu kujilimbikizia madaraka.

Hata hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana mjini Dodoma kwamba, mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa na NEC ya chama hicho ni kufanya wajumbe wa Halmashauri Kuu wachaguliwe katika ngazi za wilaya badala ya mkoa.

“Mimi nadhani hofu ya wabunge haina msingi, kwani hata kama wabunge watazuiwa ama hawatazuiwa kuwa viongozi wa chama katika ngazi hizo wanazozitaja si suala la kikatiba bali inaweza kuwa ni kanuni tu,” alisema Nape na kuongeza:

 “Hata hivyo, watapingaje kitu ambacho bado hakijawasilishwa kwenye mkutano?  Kama kuna mtu ana wazo hilo ataliwasilisha kwenye vikao, lakini nasema katiba haiwezi kumwengua mbunge katika kugombea nafasi yoyote ile, kinachoweza kumwengua ni kanuni.”

Nape alisisitiza kuwa, hadi jana hakukuwa na pendekezo lolote la kuwaengua wabunge katika kugombea nafasi za uongozi wa chama.

Hata hivyo alithibitisha kuwa uchaguzi ndani ya chama hicho unatarajiwa kufanyika kwa kuzingatia marekebisho yatakayofanywa, ambayo pia yanapendekeza wajumbe wa NEC kutoka katika jumuiya za CCM kuchaguliwa na jumuiya husika badala ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu.

Wabunge CCM
Inadaiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Kapteni John Chiligati, alipata wakati mgumu kuwashawishi wabunge hao kukubali mabadiliko hayo bila mafanikio.
“Mimi kidogo nimwambie wewe (Chiligati) ulikuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye mikakati ya kumwangusha JK (Jakaya Kikwete). Haiwezekani wakajifungia ndani na kufanya mabadiliko wanavyotaka,” alidokeza mbunge mmoja.

Taarifa hizo ziliwanukuu wabunge hao wakidai kuwa suala hilo linahitaji mjadala wa kitaifa ili kutoa wigo mpana kwa wanachama kutoa mawazo yao.

“Mnafanyaje mabadiliko bila kutushirikisha, unashika dola kwa kuwa na wenyeviti wa matawi ya CCM? Lazima uwe na wabunge ndiyo ushike dola, sasa mnatupuuza halafu mnakwenda kutuengua pembeni bila kutushirikisha, hatuwezi kukubali,” chanzo chetu kilimnukuu mmoja wa wabunge akilalamika na kuongeza:

“Kama mnasema nafasi za chini zitenganishwe, basi iwe hivyo kwa ngazi za juu kwa mwenyekiti na Rais na yenyewe itenganishwe muone moto utakaowaka.”

Hata hivyo, wabunge hao wamekubali mfumo wa kupata wajumbe wa NEC kutoka wilayani kuendelea, lakini wakakataa jinsi ya kupata wajumbe wengine na kutaka mjadala wa wazi kwa wanachama wao.
Kwa mfumo ulivyo sasa, mbali na wabunge kuruhusiwa kuchaguliwa kuwa wajumbe wa NEC, pia wana wawakilishi 20 kupitia kamati yao ambao huingia katika chombo hicho cha kufanya uamuzi ndani ya CCM.

Viti maalumu
Katika hatua nyingine wabunge wa Viti Maalumu CCM nao walitaka yafanyike mabadiliko kwenye kanuni ambayo nayo inatarajia kuwekwa ndani ya katiba ya chama hicho ya kuwataka kuwa na ukomo wa nafasi zao.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambayo yatapitiwa na CC leo, pamoja na kupitishwa na NEC kesho ni kwamba mwisho wa wabunge wa Viti Maalumu utakuwa ni miaka 10.

Kwenye Kamati ya Wabunge wa CCM, wa UWT, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Wanawake, Sophia Simba aliwashawishi wabunge waongeze kipindi hicho, lakini hoja yake iligonga mwamba.

Simba aliingiza tena ajenda hiyo katika kikao cha wabunge wote wa CCM kilichokutana juzi jioni chini ya Chiligati, lakini wazo hilo pia lilipata upinzani mkali kutoka kwa wabunge.

Kutokana na hali hiyo, Simba, Anna Abdalah, Diana Chilolo na wabunge wengine waliotumikia nafasi zao kwa vipindi viwili, huenda ubunge wao ukafikia ukomo baada ya kipindi cha sasa, hivyo wakitaka kuendelea lazima warejee kugombea nafasi hizo majimboni au kusubiri huruma ya rais katika nafasi zake za uteuzi.

Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, zinasema walioongoza kupinga kuongezwa kwa muda huo ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na yule wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambao waliungwa mkono kwa asilimia kubwa na wabunge vijana.

 “Kwa ujumla kila mahali jamaa alikuwa anagonga mwamba na tumejipanga vikali kumweleza mwenyekiti kupitia wabunge wanaoingia ndani Halmashauri Kuu na Kamati Kuu kuwa lazima mambo haya yaondolewe,’’ alisema mmoja wa wabunge.

Mbunge huyo alisema mambo mengi ambayo yalikuwa yamependekezwa na kupelekwa kwa wabunge wa chama hicho yalionekana hayana maana kwani yalikuwa yakiwanyima haki.Alisema kuwa wabunge walisimama na kumweleza Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa hawana mpango wa kuendelea kujadili mambo ya katiba ya CCM na badala yake wakamtaka aishauri Serikali ili iendelee kushughulikia kero za wananchi.


Hata hivyo, hata kabla ya kuanza kwa vikao hivyo, Rais Kikwete alikutana na wabunge hao jana usiku, kikao ambacho kilielezwa kuwa ni cha kuweka mambo sawa kabla ya kuanza kwa vikao vya juu vya chama hicho.

No comments: