KAMATI KUU CCM YABARIKI JK KUWAWAJIBISHA MAWAZIRI
Boniface Meena na Aidan Mhando
HATIMAYE
Rais Jakaya Kikwete amesikiliza kilio cha wabunge, vyama vya siasa,
wananchi wa kawaida na wanaharakati kutaka mawaziri waliohusishwa na
kashfa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) wajiuzulu baada ya kukubali kulisuka upya baraza lake.Taarifa ya
Rais Kikwete kutaka kulisuka upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa jana na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipokutana na
waandishi wa habari, Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumalizika kwa
kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.
Mawaziri ambao wizara
zao zilibainika kuwa na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma katika
ripoti hiyo ya CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni Waziri wa Nishati
na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu; Waziri wa
Fedha; Mustafa Mkulo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi,
George Mkuchika.
Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii,
Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na
Waziri wa Viwanda na Biashara; Dk Cyril Chami.
Nape alisema
Kamati Kuu iliyokutana jana ilipokea taarifa mbili ikiwemo uamuzi huo wa
Rais kulisuka upya baraza la mawaziri kutokana na ripoti ya CAG.
“Kamati
Kuu imepokea taarifa kubwa mbili, taarifa ya Kamati ya Uongozi ya
Wabunge wa CCM na Kamati ya Wabunge wa CCM kwa upande mmoja na taarifa
ya Kamati ya Uongozi ya Wawakilishi wa CCM kwa Bara na Zanzibar,”
alisema Nape.
Alisema pamoja na taarifa hizo, Kamati Kuu ilipokea
taarifa ya jinsi Rais alivyopanga kuchukua hatua za kuwawajibisha
mawaziri na watendaji serikalini na viongozi wa mashirika ya umma
waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na CAG, kamati za
kudumu za Bunge na wabunge.
“Kamati Kuu inatambua na kuheshimu
haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa Serikali yao. Inapongeza
juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa kwa uwazi
na hivyo kuibua upungufu uliojadiliwa,” alisema Nape.
Alisema
kutokana na hilo, Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais
kulisuka upya baraza la mawaziri na taasisi nyingine zilizoainishwa
katika ripoti hiyo ya CAG.
“Kamati Kuu imesisitiza utekelezaji wa
uamuzi huo wa Rais ufanywe mapema iwezekanavyo," alisema na kuongeza
kwamba Rais anaweza kuwabadilisha mawaziri na kuwawajibisha wale ambao
kutokana na uzito wa tuhuma zilizopo kwenye ripoti ya CAG, wanapaswa
kuwajibishwa.
"Taarifa ya CAG ndiyo ambayo ukiipitia inaonyesha nani atawajibishwa kutokana na uzito wa tuhuma,” alisema Nape.
Alipoulizwa lini Rais amepanga kulisuka baraza hilo la mawaziri, Nape alijibu: “Wakati wowote na haraka iwezekanavyo.”
Alisema
kabla ya Rais kutoa uamuzi huo, alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
juzi ambaye alimpa ripoti nzima ya mambo yaliyojiri bungeni.
Alisema
CCM hakijatikiswa na sakata la mawaziri hao na kwamba suala lililopo
mbele yao ni kuwawajibisha... “Tunajivunia tumelifikisha suala hili hapa
kutokana na mfumo."
Katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 10
mawaziri hao walishinikizwa wajiuzulu kiasi cha wabunge kumkalia kooni
Waziri Mkuu, Pinda baada ya ripoti hiyo ya CAG kubainisha ubadhirifu wa
fedha za umma kama ilivyowasilishwa bungeni na wenyeviti wa kamati za
tatu za Bunge.
Taarifa za ndani ambazo zilipatikana baada ya
kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika Dodoma zilieleza kuwa wabunge wa
chama hicho waliagiza mawaziri hao wajiuzulu kutokana na kushindwa
kufanya kazi zao kikamilifu.





