Saturday, April 28, 2012

BARAZA LA MAWAZIRI KUVUNJA


KAMATI KUU CCM YABARIKI JK KUWAWAJIBISHA MAWAZIRI
Boniface Meena na Aidan Mhando
HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete amesikiliza kilio cha wabunge, vyama vya siasa, wananchi wa kawaida na wanaharakati kutaka mawaziri waliohusishwa na kashfa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wajiuzulu baada ya kukubali kulisuka upya baraza lake.Taarifa ya Rais Kikwete kutaka kulisuka upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari, Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.

Mawaziri ambao wizara zao zilibainika kuwa na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma katika ripoti hiyo ya CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu; Waziri wa Fedha; Mustafa Mkulo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, George Mkuchika.

Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Waziri wa Viwanda na Biashara; Dk Cyril Chami.

Nape alisema Kamati Kuu iliyokutana jana ilipokea taarifa mbili ikiwemo uamuzi huo wa Rais kulisuka upya baraza la mawaziri kutokana na ripoti ya CAG.

“Kamati Kuu imepokea taarifa kubwa mbili, taarifa ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM na Kamati ya Wabunge wa CCM kwa upande mmoja na taarifa ya Kamati ya Uongozi ya Wawakilishi wa CCM kwa Bara na Zanzibar,” alisema Nape.

Alisema pamoja na taarifa hizo, Kamati Kuu ilipokea taarifa ya jinsi Rais alivyopanga kuchukua hatua za kuwawajibisha mawaziri na watendaji serikalini na viongozi wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na CAG, kamati za kudumu za Bunge na wabunge.

“Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa Serikali yao. Inapongeza juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua upungufu uliojadiliwa,” alisema Nape.

Alisema kutokana na hilo, Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais kulisuka upya baraza la mawaziri na taasisi nyingine zilizoainishwa katika ripoti hiyo ya CAG.

“Kamati Kuu imesisitiza utekelezaji wa uamuzi huo wa Rais ufanywe mapema iwezekanavyo," alisema na kuongeza kwamba Rais anaweza kuwabadilisha mawaziri na kuwawajibisha wale ambao kutokana na uzito wa tuhuma zilizopo kwenye ripoti ya CAG, wanapaswa kuwajibishwa.

"Taarifa ya CAG ndiyo ambayo ukiipitia inaonyesha nani atawajibishwa kutokana na uzito wa tuhuma,” alisema Nape.

Alipoulizwa lini Rais amepanga kulisuka baraza hilo la mawaziri, Nape alijibu: “Wakati wowote na haraka iwezekanavyo.”

Alisema kabla ya Rais kutoa uamuzi huo, alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi ambaye alimpa ripoti nzima ya mambo yaliyojiri bungeni.

Alisema CCM hakijatikiswa na sakata la mawaziri hao na kwamba suala lililopo mbele yao ni kuwawajibisha... “Tunajivunia tumelifikisha suala hili hapa kutokana na mfumo."

Katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 10 mawaziri hao walishinikizwa wajiuzulu kiasi cha wabunge kumkalia kooni Waziri Mkuu, Pinda baada ya ripoti hiyo ya CAG kubainisha ubadhirifu wa fedha za umma kama ilivyowasilishwa bungeni na wenyeviti wa kamati za tatu za Bunge.

Taarifa za ndani ambazo zilipatikana baada ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika Dodoma zilieleza kuwa wabunge wa chama hicho waliagiza mawaziri hao wajiuzulu kutokana na kushindwa kufanya kazi zao kikamilifu.

No comments: