
Jumla ya wanafunzi 567,567 wamefaulu mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2011na watafanyiwa mtihani wa majaribio kabla ya kuanza masomo yao rasmi katika shule walizochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Akitangaza matokeo hayo (leo), jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Philipo Mulugo (Mb.) amesema, utaratibu huo wa kufanyiwa majaribio utaanza mwakani 2012, ambapo wanafunzi waliofaulu watafanyiwa majaribio ya kupima stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Wakati huo huo, Baraza la Mtihani la Taifa limefuta matokeo yote ya watahiniwa 9,736 sawa na asilimia 1.0 waliobainika kufanya udanganyifu wakati wa mtihani huo.
“Mwanafunzi atakayebainika kuwa kajiunga na kidato cha kwanza bila kumudu stadi hizo, Mwalimu Mkuu wa shule alikotokea mwanafunzi huyo na Msimamizi wa Mtihani wakumaliza elimu ya msingi watachukuliwa hatua za kinidhamu,” amesema Waziri Mulugo.
Akizungumzia kuhusu kiwango cha ufaulu alisema kimeongezeka hadi kufikia asilimia 58.28 ukilinganisha na cha mwaka jana ambacho kilikuwa asimilia 53.52.
Aliongeza kuwa kiwango cha ufaulu wa masomo ya Kiingereza, Sayansi na Hesabu kimepanda . Somo la Kiingereza kutoka asilimia 36.47 mwaka jana hadi asilimia 46.70 kwa mwaka huu , wakati somo la Sayansi ni asilimia 61.33 mwaka huu toka asilimia 56.05mwaka jana na Hesabu asilimia 39.36 mwaka huu toka asilimia 24.70mwaka jana.
Jumla ya wanafunzi 983, 545 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwezi wa Septemba 2011 na kuonesha kuwa, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 53.52 mwaka jana hadi 58.28. Jumla ya wasichana waliofaulu ni 27,377 na wavulana ni 289,190.
Wakati huo huo, Serikali imesema, kazi ya kuhakiki madai ya walimu imekamilika tangu Desemba 2, mwaka huu na kwamba madai hayo ni kiasi cha sh. bilioni 52.
Akijibu swali lililoulizwa na waandishi kuhusu madai ya walimu, Naibu Katibu Mkuu Bw. Selestine Gesimba amesema, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 30 ni za mishahara na bilioni 22 ni za madai mengineyo.
Bw. Gesimba ameongeza kuwa, madai ya malipo mengine yataanza kulipwa mwezi huu (Desemba) na madai ya malipo ya mishahara yatalipwa ifikapo Januari 2012.
Hata hivyo alisema tayari Hazina wameshalipa bilioni 28 za madai ya mishahara kuanzia Julai mwaka jana hadi Novemba mwaka huu.
....................................................................................................................................................................
Serikali imezuia ukamataji, uingizaji na usafirishaji wa wanyama pori hai isipokuwa wadudu tu kutokana na Amri ya kuzuia ukamataji ijulikanayo kama The Wildlife Conservation (Capture of Animals) (Prohibition) Order, 2011.
Akitoa tamko hilo, Bw. George Matiko msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii amesema kutokana na Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 435 la tarehe 09 Desemba 2011 wafanyabiashara wenye vibali halali vya kumiliki na kusafirisha wanyamapori hai ambavyo hadi tarehe 18 Agosti, 2011 vilikuwa havijamaliza muda wake kisheria wanatakiwa kusafirisha wanyama hao ndani ya kipindi cha miezi mitatu (siku 90) tangu tarehe 9 Desemba 2011.
Tangazo hili la Serikali limetolewa na kutambua kuwa wakati amri ya kusitisha biashara ya wanyapori hai ilipotolewa tarehe 18 Julai 2011, kuna baadhi ya kampuni ambazo tayari zilikuwa na wanyamapori katika mazizi yao waliokuwa wamekamatwa kwa mujibu wa sheria.
Muda uliotolewa kwa wafanyabiashara ni kwa mujibu wa Kanuni za Ukamataji wa Wanyamapori za mwaka 2010 zilizotangazwa kwa Tangazo la Serikali Na. 244 la tarehe 02 Julai, 2010. Kanuni ya 12(4) na (5) ya kanuni hizo inaelekeza kuwa wanyamapori waliokamatwa kwaajili ya usafirishaji nje ya nchi kibiashara wanatakiwa wawe wamesafirishwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu kukamatwa.
Vilevile, kutokana na Tangazo hilo (Na. 435 la tarehe 09 Desemba 2011) Wizara imezuia ukamataji, uingizaji na usafirishaji wa wanyamapori hai isipokuwa wadudu tu (Class 21).
Serikali kupitia Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa matumizi mengine ya wanyamapori hai pamoja na mazao yake kwa shughuli zisizo za kibiashara na zenye manufaa kwa Taifa, kama vile utafitii, yanaruhusiwa.
No comments:
Post a Comment