Monday, February 13, 2012

KASHFA MPYA MUHIMBILI




HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, imekumbwa na kashfa nyingine inayotokana na mmoja wa madaktari wake, kumdunga sindano mtoto Imrani Iddy na kusababisha apooze mwili mzima.

Habari zilitolewa na wazazi wa Imrani, zilisema mtoto huyo amelazwa  katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, katika hospitali hiyo.


Wazazi hao walisema mtoto wao amekuwa katika chumba hicho muda wa miezi sita sasa huku akiwa anapoteza fahamu. Kwa mujibu wa habari hizo, mtoto huyo alichomwa sindano hiyo na mmoja wa madaktari katika Kitengo cha Upasuaji.


Hii ni mara ya pili kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukumbwa na kashfa ya aina hiyo ndani ya kipindi cha takriban miaka mitano iliyopita. Novemba mosi mwaka 2007, wagonjwa wawili waliokuwa wamelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), iliyoko katika hospitali hiyo, walifanyiwa upasuaji kinyume cha matatizo yaliyokuwa yakiwakabili.


Katika upasuaji huo tata, Immanuel Didas aliyekuwa anasumbuliwa na goti baada ya kupata ajali ya pikipiki, alifanyiwa upasuaji wa kichwa na Immanuel Mgaya aliyepaswa kufanyiwa upasuaji wa kichwa , alifanyiwa upasuaji wa mguu.
Katika tukio la mwaka huu lililothibitishwa na wazazi mtoto huyo wa umri wa miaka mitatu, Iramni alichomwa sindano hiyo Julai 28 mwaka jana.

Mama wa mtoto huyo Amina Mwerangi ambaye aliwahi kuwa mshindi wa mashindano ya ulimbwende  katika Mkoa wa Ruvuma mwaka 2003/04, alisema alimpeleka mtoto huyo Muhimbili ili akafanyiwe upasuaji mdogo wa nyama zilizoota puani.
"Baada ya kuchomwa sindano hiyo, mtoto alipatwa na mshtuko uliosababisha mapigo ya moyo wake kusimama. Tatizo hilo sasa limemletea mtindio wa ubongo na kupooza mwili wote," alisema Mwerangi.
Mwerangi alisema jitihada zake za kumpata daktari aliyemchoma sindano hiyo Imrani, hazikuzaa matunda na kwamba Dk Edwin aliyekuwa amfanyie upasuaji huo, hataki kujihusisha na tatizo hilo.
“Mtoto amelazwa ICU kwa miezi sita sasa huku kukiwa hakuna matumaini ya kupata nafuu, jambo la kushangaza ni kuona madaktari wakiwa hawataki kumpa rufaa ili apelekwe nje kwa matibabu zaidi,” alisema mama wa mtoto huyo.
  Alisema  katika upasuaji aliopaswa kufanyiwa, Imrani alifunguliwa jalada lenye namba IP.No.A586301 lililoeleza kuwa alikuwa na tatizo la kuota nyama kwenye njia ya hewa puani na kwamba nyama hizo zilikuwa zinamfanya apate shida katika kupumua.

Alisema mtoto huyo ambaye kabla ya kusababishiwa tatizo hilo jipya alikuwa anasomo katika Shule ya Awali ya Mtakatifu ya mjini Dodoma, alibainika kuwa na ugonjwa huo wakati alipoanza kutambaa.

“Baada ya kumpeleka Hospitali ya Muhimbili katika kliniki ya kawaida, waliniambia kuwa mtoto anapaswa kufanyiwa upasuaji mdogo ili kuondoa nyama hizo na Julai 28 mwaka jana, nilikwenda hospitalini hapo kupata huduma hiyo,” alisema Mwerangi.

 “Nilipokewa na mtoto na siku iliyofuata kwa maana ya  Julai 29 alipelekwa katika chumba cha upasuaji kufanyiwa huduma hiyo, lakini kabla ya hapo alipigwa sindano ya usingizi iliyomsababisha apate mshituko,” alidai mama huyo.

Alisema kutokana hali hiyo, mapigo ya moyo ya mtoto yalionyesha dalili za kusimama na hivyo  akahamishiwa  katika chumba cha wagonjwa wa moyo wanaohitaji uangalizi maalumu.

 “Mtoto  alilazwa katika chumba hicho  hadi Januari 24 mwaka huu, alipohamishiwa katika ICU ya kawaida ambako ndiko aliko hadi sasa,” alisema.
  Mwerangi alisema taarifa ya kitabibu  iliyotolewa baada ya kufanyiwa vipimo vya CT Scan, ilionyesha kuwa  mtoto huyo amesababishiwa mtindio wa ubongo na kwamba mwili wote umepooza.
 “Kila nikiuliza ni daktari gani aliyempiga sindano mtoto, sipewi jibu, kila mmoja anasema hajui na kwamba walimkuta tu ndani ya chumba cha upasuaji akiwa hivyo. Badala yake wananiuliza kuwa kwani  dereva akisababisha ajali na watu wakafa yeye akapona atasimama,” alisema mama wa Imrani.

Mwerangi alisema mbali na kumficha daktari aliyemchoma sindano mtoto, pia amekuwa akinyimwa ruhusa ya kumpeleka nje ya nchi kwa matatibu zaidi.
“Nilikwenda kwa Mkurugenzi wa huduma za tiba ya ugonjwa nyama, akasema  hakuwa na taarifa na akashangaa sana kusikia eti  mtoto amekuwa ICU kwa muda wote huo,”alisema.
  “Aliniambia angezungumza na madaktari waliotaka kumfanyia upasuaji mtoto. Lakini hadi sasa hakuna taarifa wala hatua zozote zilizochukuliwa,” alisisitiza mama Imrani.
 Hata hivyo alimshukuru  Dk Ulisubisya kwa kumpa ushirikiano wa karibu  licha ya ukweli kwamba si daktari aliyemhudumia mtoto.

Alisema pamoja na mambo mengine, daktari huyo ndiye aliyewezesha kupatikana kwa taarifa ya kitabibu za mtoto huyo.

Uongozi wa hospitali

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Dk Merina Njelekela, na Ofisa Uhusiano wake, Aminiel Aligaeshi, hawakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, licha ya juhudi za kuwatafuta.


Juzi mwandishi wa habari hii alikwenda kwa ofisa uhusiano ili kupata ufafanuzi wa madai hayo, lakini jitihada hizo zililigonga mwamba baada ya kukataliwa kumuona.
 Juhudi  kama hizo ziligonga mwamba pia katika kumpta Dk Njelekele ofisini kwake, kufuatia kitendo cha wasaidizi wake kumzuia mwandishi kuonana naye kwa maelezo kuwa ana kazi nyingi.
 Hata hivyo, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa hospitalini hiyo, Jeza Waziri, ambaye awali alisema hawezi kuzungumza lolote, alisema hakuwa na  taarifa kuhusu tukio hilo.






                                          RAZA APETA  UZINI




MGOMBEA wa CCM, Mohamed Raza Daramsi  jana alitangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa kumsaka Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Zanzibar.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Malimu Ally Juma  alisema Daramsi alipata kura 5,377 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Ali Mbarouk Mshimba aliyepata kura 281 na wa tatu alikuwa wa Chama Cha CUF, Salma Hussein Zarali aliyepata kura 223.

Wagombea wengine  walikuwa Khamis Khatib Vuai wa  Chama cha Tadea aliyepata kura 14 na Yussuf Rashid Mshenga  wa chama cha AFP aliyepata kura nane

Matokeo hayo ya mgombea wa CCM kupata ushindi yalitarajiwa tangu awali, lakini jipya ni kuona Chadema ikiipiku CUF ambayo wengi wanaamini kuwa ngome yake ni visiwani hapa.
Hata hivyo, Chadema jana hiyo walikataa matokeo hayo wakisema watapinga kortini na walisusa kutia saini.

Awali jana hiyo, wakazi wachache jimbo hilo, walijitokeza kupiga kura  katika uchaguzi mdogo wa kumchagua mwakilishi wa jimbo hilo kufuatia kifo cha aliyekuwa mwakilishi wake Musa Khamis Silima aliyefariki kwa ajali ya gari Oktoba mwaka jana.

Karibu watu 8,000walitarajiwa kupiga kura, lakini katika vituo kadhaa walijitokeza watu wachache.

Vyama vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi huo ni vitano ambavyo ni Tadea, CUF, AFP na CCM na Chadema.
Jana hiyo kura zilipigwa baada ya kufanyika kwa kampeni ya mwezi mmoja ambapo wagombea waliweza kujinadi kwa kutangaza sera zao na vyama vyao huku wakiomba ridhaa ya wananchi ili wawachague.

Pamoja na vyama vitano kushiriki kwenye uchaguzi huo, lakini tangu awali CCM ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kufuatia watu wengi kuiunga mkono kipindi chote cha kampeni huku vyama vya CUF na Chadema vikiwania nafasi ya pili na ya tatu.

Zoezi la upigaji kura lilianza mapema saa mbili na nusu asubuhi huku hali kwenye vituo ikiwa ni ya amani na utulivu na wananchi walijitokeza  kwa uchache kwenda kupiga kura.

Katika kituo cha Mtakawani, wakala mmoja ambaye hakujulikana ni wa kutoka chama kipi cha siasa alimzuia mtu kupiga kura na kuwaambia wasimamizi kutoka Tume ya uchaguzi akiwahakikishia kuwa yule sio mwenye kitambulisho kile licha ya picha kuonekana kufanana naye.

Hata hivyo hatua ile ilisababisha polisi waliokuwa katika kituo kile kuingilia kati na kuwataka wafuate utaratibu na kisha ofisa wa Tume ya uchaguzi ambaye hakutaka kujitambulisha akamtaka mlalamikiwa yule kuondoka eneo lile kwa kuwa kitambulisho kile hakikuwa chake na asingeweza kupiga kura.

Hata hivyo huenda idadi ya wapiga kura ikawa ndogo kuliko ile ya watu waliojiandikisha na wanaostahili kupiga kura.
Jimbo hilo linawapiga kura 8,743 waliojiandikisha na kuidhinishwa na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (Zec) lakini hadi saa 8 za mchana idadi ya wananchi waliojitokeza ilikuwa ni chini ya nusu ya wananchi waliotarajiwa kupiga kura.

Gazeti hili lilitembelea katika vituo vya Uzini A na B na kingine cha Mitakarani A na B majira ya saa 8:00 mchana jana na kuzungumza na wasimamizi wa vituo hivyo ambapo walisema vituo vyenye idadi ya wapiga kura 350 kila kimoja vilikuwa na idadi ndogo ya waliopiga kura.

“Hapa kwetu vituo vyetu viwili vina wapiga kura 350, lakini mpaka sasa tumetumia vitabu viwili na nusu na kila kitabu kina idadi ya wapiga kura 50 ,” alisema na kuongeza katika kituo cha Uzini B tayari wameshatumia vitabu vitatu ambavyo jumla ya wapiga kura ni 150 tu.

Ofisa usimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Kati, Musa Haji alisema licha ya kuonekana idadi ndogo ya waliojitokeza mpaka mchana wa jana, walitarajia idadi ya wapiga kura kuongezaka na kufikia walau watu 4,000.









 WAZIRI MKUU AJIUZULU

VYAMA vya siasa vya upinzani, vimemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ajiuzulu kwa maelezo kuwa vitisho vyake kuhusu matumizi ya vyombo vya dola  katika kushughulikia mgomo wa madaktari nchini, vilichochea maafa.Matakwa hayo ya vyama vya upinzani, yamekuja siku kadhaa baada ya Pinda kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa kufuatia mgomo huo uliomalizika wiki Alhamisi iliyopita.


Akitangaza hatua huyo, Waziri Mkuu alisema inalenga katika kutoa nafasi kwa vyombo vya dola kuwachunguza maofisa hao kwa tuhuma zinazowakabili.

Tuhuma hizo ni pamoja na kuingiza nchini vifaa duni vya kupimia virusi vya Ukimwi kutoka Korea kusini, utata katika zabuni ya kampuni inayofanya usafi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na zabuni za sare za madaktari na wauguzi katika hospitali hiyo.

Lakini jana, wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya Chadema, CUF, SAU, CCK, na TLP walisema, haitoshi kuwasimamisha Nyoni na Dk Mtasiwa pekee na kwamba kuna haja kwa Waziri Mkuu naye ajiuzulu.
Walisema Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa katika kulishughulikia mgomo huo  na kusababisha uchukue muda mrefu na matokeo maafa kwa watu wasiokuwa na hatia.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema  kilichotokea katika sakata hilo kinaonyesha jinsi namna Serikali ilivyo dhaifu na inavyoshindwa kujisimamia.

Alisema pia kushinda kuupatia mgomo huo suluhu ya haraka,  kumeonyesha jinsi Waziri Mkuu alivyoshindwa kuwajibika katika nafasi yake.
Mbowe alisema uongozi wa busara na hekima ulipaswa kuchukua nafasi katika kushughulikia mgomo huo na kwamba kwa msingi huo, hakukuwa na sababu kwa Pinda kutoa vitisho kwa madaktari.

Kiongozi huyo wa Chadema alisema madaktari  walikuwa na hoja  za msingi na kwamba kitendo cha Pinda kuwatishia kiliwakatisha tamaa.
Mbowe alisema si vizuri mambo ya kitaalam kushughulikiwa kisiasa kama ilivyofanywa na Serikali.

Kwa mujibu wa Mbowe, wazoo la kujiuzulu linapaswa pia kufanywa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda ambaye wakati mgogoro unaanza, alikuwa likizo jimboni kwake na ilimchukua wiki nzima kurudi jijini Dar es Salaam kushughulikia mgomo huo.

"Huu ni udhaifu mkubwa wa kiutendaji na mbaya zaidi waziri Pinda kaamua kuwasimamisha kazi katibu mkuu na mganga mkuu baada ya shinikizo la bunge na wala si vingine. Naamini hivi kwa sababu kwake suala hilo lilifika akatumia vitisho kisha akaagiza madaktari wa jeshi kwenda kuchukua nafasi za madaktari wa Muhimbili na mwisho wa siku ikabidi azungumze nao," alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi hao wanaendelea na utamaduni uliozoeleka serikalini wa  kusubiri maafa na baadaye kuchukua hatua.

 Alisema mtindo huo unatokana na tabia ya kulindana iliyoota mizizi katika Serikali ya CCM.
"Kamati ya Bunge ya Huduma za  Jamii, ilisafiri kutoka Dodoma hadi Dar es Saalam na kuzungumza na madaktari, wizara ya fedha na wadau wengine na ikarudi na kukutana na uongozi wa Bunge na baadaye ndio Pinda akachukua hatua za kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu na Mganga wa Mkuu wa Serikali," alisema.
Alisema Pinda anapaswa kujiuzulu kwa sababu busara yake ya  kuwatisha madaktari na kuwapeleka wanajeshi Muhimbili imechangia kuua  baadhi ya wagonjwa.

"Udaktari kulingana na kanuni zake kama usipoufanya kwa mwaka mmoja, ni lazima usome tena walau kwa mwaka mmoja kabla ya kutoa huduma, hivyo haina shaka kabisa kuwa wastaafu wa JWTZ waliopelekwa Muhimbili wamechangia vifo vya baadhi ya wagonjwa," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SAU, Paul Kyara alimtaka Pinda awajibike kwa kujiuzulu kwa maelezo kuwa alitumia vitisho badala ya kutafuta muafaka katika kushughulikia mgomo.
"Pinda aliwatisha madaktari badala ya kuangalia jinsi ya kutatua tatizo. Sasa kilichotokea kitachochea migogoro zaidi serikalini," alisema Kyara.
Kyara alielezea wasi wasi wake kuwa huenda Waziri Mkuu hana washauri wazuri na kusisitiza kuwa kimsingi, hakupaswa kutoa kauli ya vitisho kwa madaktari.

Alisema badala yake kiongozi huyo alipaswa kuwatia moyo madaktari na kuonyesha kuhusika kwake katika madai yao kama alivyofanya baadaye.
"Serikali iache siasa katika masuala ya kitaaluma na yale yanayohitaji utaalamu. Lakini haya yanayotokea yanachangiwa na kulindana na kupachikana katika nafasi ambazo kimsingi, waliowekwa hawana uwezo," alisema Kyara.


Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa, aliirushia kombora Idara ya Usalama wa Taifa kwamba imeonyesha udhaifu unaomfanya Waziri Pinda aonekane kuwa hatoshi katika nafasi yake.
“Inaonekana kuna tatizo katika vyombo vya usalama kwa sababu wao walipaswa kuliona jambo hili na kumshauri Waziri Mkuu bila kuegemea upande wowote lakini, hawakufanya hivyo na ndio maana akawa na kauli mbili tofauti katika suala moja," alisema Mnyaa.

Mbunge huyo alisema vyombo hivyo vina wajibu wa kuzuia mambo hayo kabla hayajatokea lakini, hawakufanya hivyo matokeo yake wanamweka Pinda katika wakati mgumu.

Katibu Mkuu wa CCK Renatus Muabhi, alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeonyesha udhaifu mkubwa katika kipindi chote cha mgomo wa madaktari.
 Alisema katika kipindi hicho Rais Kikwete alikuwa nje ya nchi na kwamba hata aliporudi aliona bora aende katika uzinduzi wa tawi la benki mojawapo ya kigeni, badala ya kushughulikia roho za wapiga kura wake.
"Wananchi ndio wamemchagua na matibabu ni sehemu ya haki yao ya kikatiba lakini, Kikwete kawapuuza na kwenda kufungua vitega uchumi vya wawekezaji ambao pia wanalaumiwa kwa kufilisi uchumi wa nchi," alisema Mhabi.
Katibu huyo alisema ni vema Rais Kikwete akawaomba radhi Watanzania katika kile kilichotokea katika mgomo huo, vikiwamo vifo vya wapiga kura.

Alisema vinginevyo awajibike kwa kujiuzulu na waziri mkuu wake, Pinda.
"Kisiasa kifo cha mtu mmoja ni kashfa kubwa sana kwa Serikali iliyopo madarakani kwa hiyovifo vya makumi ya wapiga kura wa chama kilichopo madarakani kutokana na mgogoro wa Serikali na watendaji wake si jambo la kuacha kama lilivyo, waombe radhi au wajiondoe," alisema Mhabi.

Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya vyama vya upinzani, Katibu wa  Itikadi  na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye simu yake iliita na kuikata na kisha kutaka atumiwe ujumbe wa maandishi.

Katibu majibu yake kwa ujumbe aliotumiwa, alisema hayupo katika mazingira mazuri ya kuzungumzia hayo.

"Nipo katika kikao cha NEC siko katika position (nafasi) ya ku-comment (kutoa maoni),” alijibu Nape kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.

Mgomo huo uliodumu kwa zaidi ya wiki mbili unadaiwa kusababisha vifo vya baadhi ya wagonjwa katika hospitali tofauti nchini.

Hata hivyo ulimalizika baada ya Waziri Mkuu, kukutana na madaktari na kuwasimamisha kazi  Dk Mtahsiwa na  Nyoni.

Hatua hiyo ilikuja baada ya madaktari hao kukaidi amri ya Pinda ya kuwataka madaktari kurejea kazini mara moja la sivyo watakuwa wamejifukuzisha kazi na kuendelea na mgomo hadi alipokutana nao na kutangaza kuwasimamisha viongozi hao wa wizara.
Awali Pinda aliwataka madaktari waliokuwa katika mgomo kurudi kazini mara moja na kwamba vinginevyo, watakuwa wamejifuuzisha kazi wenyewe.






 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika kikao chake cha siku moja chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Taifa Dr. Jakaya M. Kikwete, pamoja na mambo mengine imetoa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki. Katika kikao chake hicho kilichofanyika tarehe 12/02/2012 mjini Dodoma, NEC pia imetoa ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye kata nane zilizotangazwa kufanya chaguzi Ndogo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. 1. UBUNGE: Katika nafasi ya Ubunge kwa Arumeru Mashariki, utaratibu utakaotumika ni ule wa kupiga kura za maoni kwenye Mkutano Mkuu wa Jimbo. (i) Tarehe 13 – 18/02/2012 Kuchukua na kurejesha fomu. (ii) Tarehe 20/02/2012 Mkutano Mkuu wa Jimbo kupiga Kura za maoni. (iii) Tarehe 21/02/2012 Kamati ya Siasa ya Wilaya kujadili Wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa. (iv) Tarehe 24/02/2012 Kamati ya Siasa ya Mkoa kujadili Kutoa mapendekezo yake kwa Kamati kuu. (v) Tarehe 27/02/2012 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kufanya uteuzi wa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi. 2. UDIWANI Nafasi ya Udiwani katika kata 8 za Tanzania Bara Katika nafasi hii kura za maoni zitapigwa kwenye Mikutano Mikuu ya Matawi. (i) Tarehe 13 – 16/02/2012Kuchukua na kurejesha fomu. (ii) Tarehe 17 – 21/02/2012 Kampeni za Uchaguzi kwenye Matawi. (iii) Tarehe 22/02/2012Mikutano Mikuu ya Matawi kupiga kura za maoni. (iv) Tarehe 25/02/2012 Kamati za Siasa za Wilaya kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Mikoa. (v) Tarehe 27/02/2012 Kamati za Siasa za Mikoa kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu za Mikoa. (vi) Tarehe 29/02/2012 Halmashauri Kuu za Mikoa kufanya uteuzi wa wagombea. Katika hatua nyingine Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imepokea maelezo juu ya mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya na maelezo juu ya mgomo wa madaktari nchini. Kwa ujumla NEC imepokea maelezo hayo kutoka serikalini na kuiagiza serikali kukamilisha mchakato wa kumaliza kabisa mgogoro wa madaktari nchini na kuhakikisha migogoro ya namna hiyo inashughulikiwa mapema ili isiwe na madhara makubwa kwa wananchi. NEC imeridhishwa na jinsi mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya unavyoendelea na kuipongeza serikali kwa jinsi inavyolisimamia swala hilo. Imewataka wana CCM na wananchi wote kushiriki mchakato huo, huku wakizingatia kutunza amani na utulivu uliopo nchini. Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imewapongeza viongozi, wanachama na wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa jinsi walivyofanikisha sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi ambapo kitaifa mwaka huu zilifanyika mkoani humo. Sherehe hizo ziliandaliwa na kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu kabisa, hivyo NEC inawapongeza kwa kufanikisha sherehe hizo. Pamoja na Mkoa wa Mwanza NEC inawapongeza wanachama, viongozi na wananchi kwa ujumla nchi nzima kwa jinsi walivyofanikisha sherehe hizo za miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM kwenye maeneo yao. Imetolewa na; Nape Moses Nnauye Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa

 


No comments: