Wednesday, February 29, 2012

MAHALU AMCHOMA JK



ANIKA ALIVYOSHIRIKI KATIKA MCHAKATO KIPINDI AKIWA WAZIRI MAMBO YA NJE, ASEMA ALIKUTANA NA MAMA MWENYE NYUMBA NA KUAGIZA ALIPWE DOLA MILIONI MOJA HARAKA, AKAMPA OFA KUJA MBUGA YA NGORONGORO
Tausi Ally
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifahamu kuwepo kwa rasimu mbili za mikataba ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania, Italia.

Profesa Mahalu alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ilvin  Mgeta wakati akitoa utetezi wake dhidi ya kesi inayomkabili  ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.

Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Profesa Mahalu aliitambua barua ya Februari 20, 2002 ambayo ilikuwa ikieleza kuwa matayarisho yote ya ununuzi wa jengo la ubalozi huko Italia yamekamilika ikiwa ni pamoja na rasimu mbili za mikataba.

Mahalu alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wakati yeye akiwa Balozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kulikuwa na rasimu mbili za mikataba na kwamba aliwahi kuwasiliana na wizara hiyo juu ya mikataba hiyo.

Alidai kuwa Desemba 2001, Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikwenda Rome, Italia kwenye Mkutano wa SADC na alipokuwa huko, ubalozi ulifanya mpango atembelee jengo hilo lililopendekezwa kununuliwa kwa ajili ya ofisi ya ubalozi.

“Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia ilifanya mipango yote kwa kumpa utaratibu na usalama Kikwete ambapo alikwenda kutembelea jengo hilo na kukutana na mama mwenye jengo,” alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa kabla ya mazungumzo na mwenye nyumba, mtoto wa mama huyo, Alberto alimtembeza Kikwete kwenye jengo hilo ndani na nje na baadaye mazungumzo hayo yaliendelea.

Balozi Mahalu alisema baadaye mazungumzo kati ya Kikwete na mama huyo yaliendelea na Alberto alikuwa akitafsiri, kwa sababu mama yake hakufahamu lugha ya Kiingereza.

Profesa Mahalu alidai kuwa katika mazungumzo hayo, Kikwete alimwuliza mama huyo: “Hivi ni kwa nini kunakuwa na mikataba miwili?” na mama huyo alimjibu kuwa hiyo ni kawaida kwa Italia ukitaka kununua jengo kwa bei nafuu.

Profesa Mahalu aliendelea kudai kuwa baada ya kupewa jibu hilo,  Kikwete hakuzungumza tena zaidi ya kucheka na kwamba mwenye jengo alimkumbusha kuhusu malipo ya awali ya dola milioni moja za Marekani ambapo aliafiki na kuahidi kuwa zingelipwa kabla ya mwisho wa mwaka 2001.
Profesa Mahalu alidai pia kwamba Kikwete alimweleza mama huyo kuwa atalishughulikia suala hilo baada ya kurejea Dar es Salaam na kumshukuru kwa kuwauzia jengo zuri.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kusema maneno hayo, alimgeukia na kumwambia: “Costa ni vizuri tupate hela tumlipe huyu mama watu wengine wasije wakachukua hili jengo.”

Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kumshukuru mama huyo kwa ukarimu wake, alimkaribisha Tanzania awe mgeni wa Wizara ya Mambo ya Nje yeye na mumewe na kwamba watampeleka Ngorongoro.

“Tulipokuwa njiani tukirudi hotelini alipofikia Kikwete akiwa kwenye gari alimpigia simu Kibero akimuagiza afanye utaratibu wa kulipa Dola milioni moja kama malipo ya awali ya jengo hilo,” alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa baadaye alimwagiza (Profesa Mahalu) aje Dar es Salaam kufuatilia mpango huo wa malipo ya awali ya ununuzi wa jengo hilo.

Awali, Profesa Mahalu akiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa alidai kuwa anaitambua ripoti ya uthamini wa jengo hilo la ubalozi nchini Italia uliofanywa na Kimweri kutoka Wizara ya Ujenzi  aliyekwenda Rome Julai 15 hadi 26, 2001 kwamba jengo lilikuwa na gharama ya Sh6 bilioni.

Pia alizitambua ripoti za uthamini wa jengo hilo ambazo ni ile ya mama mwenye nyumba ambayo ilionyesha kuwa jengo hilo lilikuwa na thamani Sh5.500 bilioni na ripoti ya uthamini iliyofanywa na Serikali ya Italia iliyoonyesha kuwa jengo lilikuwa na thamani ya Sh11.117 bilioni.









CHILIGATI ATISHIA KUJIUZULU 

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati juzi alitaka kujiuzulu ujumbe wa Sekretarieti ya chama hicho mbele ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kutokana na kukerwa na kile alichokiita kuvuja kwa siri za kikao cha sekretarieti hiyo  iliyoketi mwishoni mwa wiki kujadili mchakato wa kura za maoni kuelekea uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki.

Kikao hicho cha Sekretarieti kilichoketi Dar es Salaam, kilikotoka na pendekezo la kutaka mshindi wa kura za maoni Sioi Sumari atoswe kutokana na sababu kuu mbili, utata wa uraia wake kutokana na kuzaliwa Kenya na kutoungwa mkono na wagombea wenzake.

Sekretarieti hiyo ambayo ilitoa mapendekezo hayo kwa Kamati Kuu (CC) ya CCM, pia ilitoa angalizo kwamba kama Sioi angepitishwa, chama kingekuwa katika hatari ya kuwekewa pingamizi kutokana na madai hayo ya utata wa uraia na pia, vigogo wengine wangekisaidia Chadema ili kishinde uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Aprili Mosi, mwaka huu.

Siku iliyofuta mkakati huo ulivuja katika vyombo vya habari siku ambayo pia kulikuwa na kikao cha CC na ndipo Chiligati  alipolalamika mbele ya Mwenyekiti Kikwete akidaiwa kusema: “Haiwezekani mambo tuliyojadili jana (siku ya kikao) yaandikwe katika magazeti neno kwa neno.”

Alipoulizwa jana kuhusu tishio lake la kutaka kujiuzulu Chiligati alisema: “Mambo ya Ngoswe mwachie Ngoswe mwenyewe.” Mahojiano yake na mwandishi wetu yalikuwa kama ifuatavyo:

Swali: Salaam ndugu Chiligati. Kwanza heri ya mwaka mpya.
Jibu: Nzuri, nashukuru na wewe pia.

Swali: Nimesikia kuwa juzi ulitaka kujiuzulu ujumbe wa sekretarieti kutokana na kuvuja siri za kikao chenu cha juzi cha mchakato wa kura za maoni wa Arumeru Mashariki je, msimamo wako ukoje hadi sasa hivi?
Jibu: Bwana wewee! Sikia, hayo ni mambo ya ndani ya vikao. Mambo ya ngoswe mwachie ngoswe mwenyewe!

Swali: Sawa, natambua ni la vikao vya ndani vya chama, lakini huoni kuvuja kwa siri za vikao vyenu kunaonyesha sekretarieti imegawanyika?
Jibu: Nakwambia hivi, hayo ni mambo ya ndani ya vikao. Kwani wewe mbona hutuambii mambo ya nyumbani kwako na mkeo?

Swali: Hujaniuliza, ungeniuliza ningekwambia. Lakini, je, sasa kama siri zitaendelea kuvuja msimamo wako utakuwa ni upi?

Jibu: Haaah...! Wewe bwana shughulika na ya kwako, haya hayakuhusu. Haya ni sawa na mambo ya ndani ya nyumba, ni yetu wenyewe tutayazungumza kwenye vikao vyetu.

Swali: Lakini, tayari mmeweza kubaini ni vipi siri za vikao vyenu zinavuja na labda mmejua ni nani anayezivujisha?
Jibu: Nasema tuachie wenyewe, hatutaki utuingilie. Nasisitiza tena kitu kimoja, hilo halikuhusu endelea na mambo yako.

Wakati Chiligati akijibu hayo, taarifa kutoka ndani ya kikao hicho cha CC, zilisema kwamba baadaye Rais Kikwete aliitaka sekretarieti hiyo yenye watu tisa ijiangalie yenyewe kujua nani anavijisha taarifa za vikao.

Katika kikao hicho sekretarieti, mbali ya kumwekea vikwazo Sioi, kilitaka Sarakikya ambaye alishika nafasi ya pili apitishwe na chama.

Mkutano Mkuu wa jimbo hilo uliofanyika Februari 20 ulimchagua Sioi, mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Jeremiah Sumari kwa kura 361, akifuatiwa na William Sarakikya aliyepata kura 259, Elishilia Kaaya (176), Elirehema Kaaya (205), Anthony Musari (22) na Moses Urio (11).

wakati huo huo
MGOMBEA Ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chadema, anatarajiwa kujulikana leo, mara baada ya kumalizika zoezi la kupigiwa kura kwa wagombea saba ambao wamejitokeza kuchukua fomu.Katibu wa Chadema wilaya ya Arumeru,  Totinan Ndonde, akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, alisema wajumbe 1,100 wa jimbo hilo watashiriki kwenye mkutano mkuu maalum wa kuchagua mgombea.

Alisema mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Meru Plaza na utasimamiwa na viongozi wa chama hicho mkoa wa Arusha.

Aliwataja wagombea ambao watachuana kuwa ni Joshua Nasari ambaye pia alishiriki uchaguzi uliopita, Anna Mughwira,Rebeca Mungwishi, Samweli Shamim na  Godlove Tema.

Wengine ni Yohane Kimuto na aliyekuwa mgombea wa CCM na kumbwagwa katika kura za maoni ndani ya chama hicho, Mwalimu Anthony Musari.

"Taratibu zote zimekamilika za mkutano huo na leo Sekretarieti ya Wilaya na Kamati ya Utendaji inakutana kupitia fomu za wagombea wote kabla ya kupeleka majina kwenye mkutano mkuu," alisema Ndonde.

Alisema mara baada ya kikao cha leo, Machi 3 Kamati Kuu ya Chadema itakutana hapa Arumeru na kuidhinisha jina moja la mgombea kabla ya kuanza kampeni Machi 9.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa Chadema, Ndonde alisema chama hicho hakina hofu na mgombea yoyote wa CCM ambaye atashinda kesho katika kura za maoni.

Katibu huyo alisema Chadema wana uhakika wa ushindi katika uchaguzi huo, bila kujali ni mgombea yupi wa CCM apitishwe.

"Sisi tuna uhakika wa ushindi aje Sarakikya au sioi, tumejipanga kulinda kura zetu kwa gharama yoyote tofauti na uchaguzi uliopita," alisema Ndonde.

Katika hatua nyingine,Chama cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa Arusha, kimewataka viongozi wa chama hicho mkoani Arusha kuacha kuingilia uchaguzi huo ili kuwapa fulsa wanaccm wa Arumeru kuchagua mgombea wao.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM mkoa, Loota Sanare akizungumza na mwananchi jana, alisema baadhi ya viongozi wa CCM na Jumuiya yake, ambao wanaonekana kuingilia sana maoni ya wana Arumeru wanapaswa kukaa kimya sasa.

"Tuwaache wachague mbunge wao, haya makundi hayana faida kwa chama chetu, kwanza hao wanaopiga kelele hana hata kura," alisema Sanare.

Kauli hiyo ya Sanare inakuja huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa kwa viongozi wa chama hicho na jumuiya zake kuhusiana na maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM  kutangaza kurejewa kura za maoni kwa wagombea wawili, William Sarakikya na Sioi Sumari.

Habari za uhakika toka ndani ya viongozi hao, wakiwepo viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Arusha na Wilaya ya Arumeru, zimebainisha kuwa mgawanyiko huo unatokana na kila kundi kuazimia kutomuunga mkono mgombea wa kundi jingine atakayeshinda.

"Hali sio nzuri kwani matamko ya hivi karibuni ya viongozi wa UVCCM mkoa, yanaonekana kumuunga mkono mgombea mmoja wakati pia baadhi ya viongozi wa CCM mkoa wanaonekana kumpinga mgombea huyo jina linahifadhiwa," alisema kiongozi mmoja.

Kiongozi huyo, alisema uhasama wa makundi hayo, ambayo ni ya muda sasa ndani ya CCM mkoa wa Arusha, huenda ukasababisha CCM kushindwa.

"Hali kama hii ilitokea katika jimbo la Arusha ambapo kuna kundi lilikuwa likimpinga mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian na lingine likimuunga mkono na hivyo alishindwa na chadema," alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, alitoa wito kwa Kamati Kuu ya CCM kuacha kuyumba katika maamuzi kwani haikupaswa kurejesha tena majina mawili kwani walikuwa na taarifa na sifa za wagombea wote hivyo walipaswa kuteua jina moja tu. 




NYARAKA MPYA ZA MASABURI 
MSUGUANO kati ya wabunge wa Dar es Salaam na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, umeibuka upya baada ya wabunge hao kusema wamepata nyaraka mpya za tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria katika suala la ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Kamati ya Wabunge hao waliokutana jana kwa dharura kujadili nyaraka hizo, imepanga kutoa taarifa kuhusu uamuzi na maazimio ya kikao na hatua ambazo watachukua leo.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Kamati hiyo, John Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, ilisema walikutana kwa dharura chini ya uenyekiti wa Abbas Mtemvu, Mbunge wa Temeke.

“Wabunge wa Dar es Salaam wanaendelea na kikao cha kupitia nyaraka zote na kufanya uamuzi wa hatua za kuchukua na taarifa juu ya hatua hizo itatolewa kwa umma baada ya kumalizika kwa mkutano unaoendelea,” Mnyika alisema jana.

Wabunge walioshiriki mkutano huo ni Mtemvu (Mwenyekiti), Mnyika (Katibu), Halima Mdee, Mussa Zungu, Idd Azzan, Neema Mgaya Hamid, Suzan Lyimo, Zarina Madabida, Faustine Ndugulile, Phillipa Mturano na Eugene Mwaiposa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyaraka ambazo Kamati hiyo imepokea ni pamoja na barua ya UDA ya Januari 26 yenye kumbukumbu namba CBA/Reg/01/UDA ambayo inataka dola za Marekani 133,125 zitolewe kutoka akaunti ya UDA ambayo ilishaagizwa awali fedha zisitoke kinyemela.

Waraka mwingine uliojadiliwa ni wa kikao kinachodaiwa kuwa cha wanahisa wa UDA cha Februari 13 ambacho inadaiwa kilifanywa na Meya Masaburi akiwa Mwenyekiti pamoja na Robert Kisena ambaye anatambulishwa kwenye muhtasari huo kama Mwenyekiti Mtendaji wa UDA na Katibu wa Bodi ya UDA.

Wabunge hao wanakishutumu kikao hicho pamoja na mambo mengine, kuwa kimefanya uamuzi haramu wa kubadili waweka saini katika akaunti ya UDA iliyozuiwa kwa lengo la kuwezesha fedha kutolewa kinyemela na Simon Group.

Wanadai kwamba Meya Masaburi kwa kushirikiana na Simon Group wameshirikiana kwa mara nyingine kukiuka uamuzi wa mamlaka mbalimbali na sheria na kanuni.

Kwa mujibu wa wabunge hao, Januari 9, Baraza la Madiwani wa Jiji lilipitisha maazimio kuhusu mgogoro unaoendelea katika UDA mojawapo ikiwa ni pamoja na kufanyika uchunguzi wa kughushiwa kwa barua iliyomwelekeza Simon Group Limited kulipa awamu ya pili ya malipo kwa kutumia akaunti ya Mwenyekiti wa Bodi ya UDA na kwamba suala lipelekwe kwenye vyombo husika kwa ajili ya kubaini ukweli na hatua kali zichukuliwe dhidi ya aliyeghushi.

Taarifa hiyo iliongeza, kwamba Baraza la Madiwani liliazimia kuwa uthamini wa hisa uliotumiwa katika kumwuzia hisa Simon Group, haukuwa halisi hivyo hisa zote zifanyiwe uthamini upya ili ziuzwe kwa bei inayostahili.

Ilielezwa pia kuwa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, liliazimia kuwa Simon Group asitambuliwe kama mwanahisa mkuu katika UDA na hivyo kuazimia kuwa iteuliwe Bodi ya muda itakayosimamia utekelezaji wa mkataba kati ya UDA na Simon Group.

Taarifa iliendelea kueleza, kwamba Baraza lilimteua Mwaiposa kuwa mjumbe wa Bodi hiyo akiwakilisha Halmashauri ya Jiji na Meya Masaburi kinyume na maazimio ya mkutano wa Januari 9, akashiriki kikao cha Bodi ya UDA Februari 13 na kudaiwa kufanya uamuzi wa kubadili waweka saini wa akaunti ili fedha zihamishwe.

Agosti 4 mwaka jana, wabunge wa Dar es Salaam walikutana Dodoma na kutoa tamko la kueleza kile walichosema ni kusikitishwa na tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa UDA.

Tuhuma za wabunge hao kwa Masaburi ziliibuka mwaka jana ambapo Meya huyo alilazimika kutumia kauli kali baada ya wabunge hao kumtaka ajiuzulu kupisha uchunguzi akisema wabunge hao baadhi yao wanashindwa kufikiri kwa kutumia vichwa na badala yake wanatumia makalio.

  



UMRI WA URAIS UWE MIAKA 35 
MBUNGE wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe wametaka umri wa kugombea urais wa Tanzania uanzie miaka 35 badala ya 41 kama ilivyo sasa.

Wakizungumza kwenye Kongamano la Katiba na Vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Femina HIP, Dar es Salaam jana, Zitto na Makamba pia walitaka umri wa kupiga kura uanzie miaka 16 badala ya 18.

Akichangia hoja, Makamba alisema ili kugombea urais katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, raia husika anatakiwa kuwa na umri wa miaka 35.

“Hatutakuwa tumeanza sisi kwa sababu nchi nyingi duniani nafasi ya urais inagombewa kuanzia miaka 35, kwa hiyo vijana tuangalie suala hilo katika mchakato wa Katiba Mpya inayokuja,” alisema.

Makamba alisema Katiba Mpya inayokuja iwawezeshe vijana kupiga kura wakiwa na umri wa miaka 16 badala ya 18: “Umri wa kuanzia miaka 16 unatosha kabisa kuchanganua ni kiongozi wa aina gani anafaa kuchaguliwa.”

Kauli ya Makamba iliungwa mkono na Zitto ambaye alizitaja nchi za Kenya, Uganda na Burundi kuwa urais unagombewa kuanzia miaka 35.

“Hata sisi Tanzania wagombea wetu wanaweza kugombea wakiwa na umri wa miaka 35 kama zilivyo nchi za wenzetu ili kuwapa vijana nafasi za kuongoza nchi,” alisema na kuongeza kuwa anamwunga mkono Makamba katika suala hilo.

Zitto akichangia hoja, pia aliunga mkono umri wa kupiga kura kuwa miaka 16 akisema hiyo itawapa nafasi vijana wengi kushiriki katika kuchagua viongozi wao.

“Zamani umri wa kupiga kura ulikuwa miaka 21, ukashushwa ikawa miaka 18, kwa wakati tulionao sasa, uwezo wa vijana ni mkubwa, wanaweza kuchagua viongozi wakiwa na miaka 16,” alisema.

Hata hivyo, Zitto alitoa angalizo kwa vijana akisema katiba pekee haiwezi kuwaletea maendeleo... “Vijana wasisubiri Katiba Mpya kuwa ndilo litakuwa suluhisho la matatizo bali, itaweka mazingira rafiki kwa vijana wanaojishughulisha.”

Aliwataka vijana wa Tanzania wasikwepe kujadili Katiba Mpya na kuwachia wanasiasa kwani jukumu hilo ni la kwao pia.

“Wanasiasa muda mwingi wanajadili mambo yanayohusu maslahi yao kama vile muda wa kukaa madarakani lakini, mambo yanayowahusu vijana yatajadiliwa kwa ufanisi na vijana wenyewe,” alisema  Zitto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza, Rakesh Rajani alisema vijana wanapaswa kuyapa kipaumbele masuala yanayohusu elimu kwa sababu huo ndiyo urithi usiohamishika.

“Elimu ndiyo kila kitu. Mnapojadili katiba angalieni mambo ambayo mnaweza kuyaweka katika Katiba Mpya,” alisema Rajani.

Meneja Uhusiano wa Femina HIP, Lilian Nsemwa alisema lengo la kuandaa kongamano hilo ni kuwawezesha vijana kutumia haki yao ya kushiriki katika mchakato wa kupata Katiba Mpya. 


 

No comments: