NI MAAZIMIO YA KAMATI KUU, YASEMA KUYUMBA KWA UCHUMI KUNATOKANA NA RAIS KUWA NA WASHAURI WABOVUBoniface Meena
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kulivunja Baraza la Mawaziri kwa maelezo kwamba limeshindwa kumshauri hivyo kusababisha hali ngumu ya maisha na kuyumba kwa uchumi wa nchi huku, migogoro ikiendelea kushamiri.Tamko hilo la Chadema linakuja kipindi ambacho tayari madaktari wametoa siku tatu kwa Serikali wakitaka kung'olewa kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya kutokana na kushindwa kusimamia sekta ya afya nchini.
Akisoma maazimio ya kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliyoketi juzi jijini Arusha, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, alisema Chadema pia kinamtaka Rais Kikwete kufumua maeneo mengine ya Serikali yake kwa kuwa mfumo wake ni mbovu usiokidhi haja ya kutekelezwa kwa majukumu yake.
Mnyika akisoma maazimio hayo jijini Dar es Salaam jana alisema, "Kamati Kuu haijaridhishwa na jinsi Serikali inavyoshughulikia suala la uchumi na hali tete ya kisiasa ikiwa ni pamoja na migogoro mbalimbali na hiyo inatokana na uwezo mdogo wa mawaziri wa JK."
Alisema CC ya Chadema haijaridhishwa na jinsi Serikali ya Rais Kikwete inavyoshughulikia mambo mbalimbali nchini na hilo linatokana na mkuu huyo wa nchi kukosa washauri wazuri katika baraza lake la mawaziri.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo alisisitiza, "Rais aanze na baraza lake la mawaziri kwa kulivunja kisha aende kwenye ngazi mbalimbali ambazo ameteua viongozi wabovu, awaondoe."
Alisisitiza, "Na hii inatokana na katiba tuliyonayo kumpa nafasi ya kuchagua watu kadri anavyotaka."
Mnyika alifafanua kwamba ili kupunguza makali na machungu kwa wananchi yanayosababishwa na uongozi huo mbovu, ni lazima Rais aanzie kwenye chombo chake kinachomshauri ili aweze kurekebisha mfumo mbovu uliopo.
"CC imezungumzia suala la migogoro inayotokea nchini na kuona kuwa Serikali inashindwa kushughulikia vyanzo vya migogoro hiyo. Hivyo ni lazima ishughulikie vyanzo vya migogoro na kuacha masihara kwenye hilo,"alisema Mnyika.
Mnyika alisema kutokana na hali ya uchumi na siasa kuwa tete CC imeamua kuwa Baraza Kuu la Chadema litakalokaa Aprili mwaka huu lijadili hali hiyo na kutoa mapendekezo kwa Serikali jinsi ya kurekebisha mambo kama Rais hatalivunja baraza hilo ambalo limekuwa mzigo kwa nchi.
Kuhusu Katiba
Akizungumzia msimamo wa CC kuhusu utoaji wa maoni ya marekebisho ya Katiba, Mnyika alisema wametambua kuwa marekebisho yaliyofanyika kwenye mkutano wa Bunge wa ulioisha Februari 10 mwaka huu kama ni ya awali hivyo CC inataka Serikali kuendelea na awamu ya pili ya mchakato huo.
"Taarifa kuhusu suala la katiba CC inatambua kuwa marekebisho yaliyofanyika kwenye mkutano wa Bunge ni ya awali hivyo inataka Serikali kuendelea na awamu ya pili na marekebisho yake kufanyika Bunge lijalo la Aprili mwaka huu,"alisema Mnyika.
Alisema CC imeamua kuwa Chadema itaendelea kutoa elimu ya marekebisho ya katiba kwenye mikutano yake, ili kuwafungua wananchi waweze kutoa maoni kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba mpya.
Mnyika alisema kutokana na wito wa Rais Kikwete kutaka majina kutoka kwa vyama ya watu watakaoingia katika tume ya mchakato wa katiba, Chadema imekaribisha maombi na mapendekezo ya watakaotaka kuingia kwenye tume hiyo.
"Kama Serikali ilivyotamgaza kuanza kwa tume hiyo kila chama kimetakiwa kuwa na wawakilishi watatu, Chadema inakaribisha maombi na mapendekezo na mwisho wa kupokea maombi hayo ni Machi 11 mwaka huu ili tuweze kufanya utaratibu,"alisema Mnyika.
Uchaguzi wa chama, Arumeru
Mnyika alisema Baraza Kuu la Chadema litakaa Aprili 29 mwaka huu na kutangaza tarehe za kufanyika kwa uchaguzi wa ndani wa chama kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.
Alisema pia Baraza Kuu litapitisha bajeti ya mpango mkakati wa muda mrefu wa chama hivyo viongozi wote wa chama walioko katika ngazi mbalimbali wajiandae kuwasilisha maoni yao.
"Kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama CC imeamua Baraza Kuu lifanyike Aprili 29 mwaka huu na kwamba nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kitongoji, kata kwenda juu zitawaniwa,"alisema Mnyika.
Kuhusu bajeti ya uchanguzi mdogo wa ubunge jimbo la Arumeru Mashariki, Mnyika alisema chama kimeamua kuwa kampeni za uchaguzi huo ziendeshwe kwa nguvu ya umma bila kutegemea ruzuku za chama.
Alisema chama kimejipanga kupata misaada kutoka kwa wananchi wa Arumeru na wananchi wengine nchini katika kuhakikisha hakitumii ruzuku ya chama kwenye uchaguzi huo.
"Kampeni za Arumeru zitaendeshwa kwa nguvu ya umma ikiwa ni pamoja na kupata fedha za wananchi kote nchini na si kutegemea ruzuku za chama bali za wananchi kwa ujumla na hasa Arumeru,"alisema Mnyika.
Alisema chama kimeteua watu kadhaa wa kuangalia jinsi gani ya kupata fedha hizo za nguvu ya umma na kile kiasi ambacho kitahitajika kuongezeka chama kitatangaza kiasi gani kitatumika.
TISHIO LA MGOMO WA MADAKTARI
WAKATI madaktari wakisisitiza watagoma kesho kushinikiza kujiuzulu kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya, mawaziri hao jana walijifungia kwenye ofisi zao siku nzima, kuwakwepa waandishi wa habari.Jana waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, walipiga kambi makao makuu ya wizara hiyo jijini Dar es Salaa kutaka kujua msimamo wa Dk Mponda na Dk Nkya, kuhusu madai hayo ya madaktari, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya viongozi hao kujifungia ofisini tangu saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana waandishi walipoanza kuondoka.
Katika Ofisi ya Waziri Mponda, wanahabari walielezwa kuwa waziri hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwa sababu liko juu ya uwezo wake.
“Nataka mfahamu kuwa waziri anajua uwepo wenu, lakini hayuko tayari kuzungumza na waandishi wa habari, hawezi kuzungumzia suala hilo sababu lipo juu ya uwezo wake,” alisema Mmoja wa maofisa katika ofisi ya Waziri Mponda.
Pia katika Ofisi ya Dk Nkya waandishi walipoingia walikutana na mmoja wa wasaidizi ambaye alitoa kauli kama ya mtangulizi wake.Baada ya waandishi kusubiri kwa muda mrefu, ilipofika saa saba mchana, Ofisa katika Ofisi ya Waziri wa Afya, aliwaeleza kuwa angerudi tena ofisini kumshauri Waziri Mponda atoke ili aweze kuzungumza na wandishi hao.
Lakini, baada ya muda alitoka Msemaji wa Wizara hiyo aliyekuwa kwenye mkutano wa wakurugenzi wa Idara zote za Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja na kusisitiza, kuwa mawaziri hawakuwa na cha kusema juu ya suala hilo kwani liko juu ya uwezo wao.“Suala la madaktari linajadiliwa katika ngazi za juu, mawaziri hawawezi kutoa maoni wala tamko lolote juu ya jambo hili,”alisisitiza Mwamwaja.
Msimamo wa madaktari
Jana, Rais wa chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi alisisitiza msimamo wa madaktari hao waliootoa mwishoni mwa wiki kuwa watagoma kesho endapo mawaziri hao hawatakuwa wamejiuzulu.
“Madaktari walishapitisha hili kwenye kikao chao, msimamo wao ni ule ule kwamba wao hawataendelea kufanya kazi, ikiwa mawaziri hao watakuwa hawajajiuzulu ifikapo Jumatano (kesho).Mwishoni mwa wiki iliyopita madaktari walitoa tamko kumtaka Rais Jakaya Kikwete awawajibishe mawaziri hao vinginevyo, wataanza mgomo kesho.
Madaktari wanawatuhumu kuwa viongozi hao kuwa chanzo cha mgomo uliotangazwa Januari 23, ambao ulisababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kuathirika.Pamoja na msimamo huo wa madaktari hadi jana, mawaziri hao hawakuonyesha dalili yoyote ya kuwajibika wenyewe.
Wizarani hapakaliki
Msemaji huyo akisema hayo, jana ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Afya hiyo ulitawaliwa na vikao vya muda mrefu vilivyohusisha wakurugenzi wote wa wizara hiyo.
Habari za ndani zinasema wakurugenzi hao walikutana kujadili sakata hilo na namna watakavyokabiliana na tisho la mgomo huo.“Wakurugenzi wote wa Idara za Wizara wapo ndani ya kikao na wananendelea na mkutano chini ya Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk Dolnald Mbando, wanajadili suala la Madaktari, wanatafuta namna watakavyokabiliana na tishio la mgomo,” kilisema chanzo hicho.
Akizunguzia hilo Mwamaja alikiri kuwepo kwa kikao hicho, lakini akabainisha kuwa kilikuwa cha uongozi wa Wizara na walikuwa wakijadili masuala mbalimbali yanyohusu wizara hiyo na si mgomo wa madaktari.
“Nikweli kulikuwa na kikao hapa wizarani, hiki ni cha menejimenti walikutana kujadili mambo mbalimbali, lakini hayahusiani na mgogoro wa madaktari,” alisema Mwamaja.
UCHAGUZI ARUMERU
WAGOMBEA wa vyama vitano vya upinzani, walijitokeza jana kuchukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki kimyakimya.
Wagombea hao, akiwamo mgombea wa Chadema, Joshua Nasari aliyesindikizwa na Meneja wa kampeni wa chama hicho, Vicent Nyerere ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Musoma mjini, walikabidhiwa fomu hizo jana na Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi.
Baada ya kuchukua fomu mgombea huyo wa Chadema ambaye aliandamana pia na Mratibu wa chaguzi za Chadema, Basil Lema ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, walitembelea Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo,Mercy Silla na kumsalimia.
Wagombea wengine waliochukua fomu, Abraham Chipaka wa Chama cha TLP, Shabani Moyo Kirita wa Chama cha SAU , Charles Msuya kutoka Chama cha UPDP na Mohamed Abdalah Mohamed wa Chama cha DP mara baada ya kukabidhiwa waliondoka.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Kagenzi alisema wagombea wote hao, walifika katika ofisi za tume na barua za uteuzi wa vyama vyao kama ambavyo taratibu zinaruhusu.
"Tunatarajia wagombea zaidi wajitokeze leo na kesho(leo) kwani muda wa mwisho wa kuchukua fomu na kurejesha ni Mach 8,"alisema Kagenzi.
Habari kutoka ndani ya CCM zinaeleza mgombea wa chama hicho, ambaye alikuwa jijini Dar es Salaam, anatarajia leo kuchukua fomu saa 5:00 asubuhi.
Nasari atoa vipaumbele vyake.
Akizungumza mara baada ya kuchukua Fomu, Nasari alisema ana imani kubwa ya kushinda na akichaguliwa kipaumbele chake kitakuwa ni kuondoa migogoro ya ardhi, kero za afya, maji, elimu na miundombinu.
"Nimekuwa nikisema Meru tuna ardhi ya kutosha, hakuna sababu ya watu kuhamishwa, kwani kuna mashamba makubwa yanamilikiwa na watu wachache, pia tutasimamia sera za kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata," alisema Nasari.
Uchaguzi huo, unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge, Jeremiah Sumari na utafanyika Aprili mosi kwa kushirikisha wapigakura 127,000 wa tarafa tatu za jimbo hilo lenye kata 17.
Msimamizi uchaguzi anawajua Chadema
Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Meru, Trasias Kagenzi, anaweka historia ya kusimamia uchaguzi wa mdogo wa pili ndani ya mfumo wa vyama vingi kwani pia alikuwa msimamizi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime.
Katika uchaguzi huo uliotawaliwa na vurugu kubwa, Wagombea wa Chadema wa ubunge, Charles Mwera na Udiwani wa Kata ya Tarime mjini John Heche wote walishinda kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehemu Chacha Wangwe.
Akizungumzia uchaguzi wa Tarime na sasa Meru, Kagenzi alisema ana imani uchaguzi wa Meru utakuwa na usalama na hautakuwa na vurugu kama za Tarime.
"Sidhani kama huku kutakuwa na vurugu kama zile, nimewaona Wameru hawapendi vurugu", alisema Kagenzi.
Kwa upande wake mratibu wa Uchaguzi wa Chadema, Basil Lema ambaye pia alikuwa akiratibu uchaguzi wa Tarime, alisema wana imani kubwa na Kagenzi kwani sasa ni mzoefu wa chaguzi ndogo.
"Huyu Mkurugenzi tunabahati naye sana kwani kila eneo ambalo tumekuwa na uhakika wa ushindi tumemkuta," alisema Lema
CCM: hatutambui
tuhuma za rushwa
Wakati huohuo, Meneja Kampeni wa CCM katika Jimbo la Arumeru Mashariki, Mwigulu Nchemba amesema chama hicho, hakitambui tuhuma za kusambaza rushwa ambazo zilikuwa zinamkabili Siyoi Sumari ambaye kateuliwa na chama hicho kugombea Jimbo la Arumeru Mashariki na hivyo ni msafi.
Akizungumza jana, Nchemba ambaye ni Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM na Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama hicho, alisema CCM inaongozwa kwa kufuata misingi ya sheria hivyo hawajawahi kupata taarifa ya Sumari kutiwa hatiani.
"CCM tunaongozwa kwa kufuata sheria, hizi tuhuma za rushwa hazijachunguzwa na CCM kwani hatuna chombo hicho hivyo mgombea wetu ni safi," alisema Nchemba.
Meneja huyo, alisema kazi kubwa iliyokuwa inafanyika katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, ilikuwa ni kumtafuta mgombea sahihi wa chama hicho na sasa amepatikana.
Wakati wa mchakato wa marejeo ya kura za maoni Makada watatu wa chama hicho, Katibu wa Itikadi na uenezi CCM Wilaya ya Nyamagana ambaye aligombea pia jimbo hilo, Elirehema Kaaya, Katibu wa UVCCM Monduli Ezekiel Mollel na Diwani wa Kata ya Mbuguni, Thomas Mollel maarufu kama Askofu, walikamatwa kwa mahojiano kutokana na tuhuma za rushwa.
Makada hao wa CCM, walidaiwa kuwa katika kambi ya Siyoi hata hivyo baada ya mahojiano waliachiwa na wote walikanusha tuhuma hizo na kueleza ni sehemu ya siasa chafu za makundi zilizopangwa kuwachafua.
Azungumzia mpasuko ndani ya CCM Arusha
Akizungumzia mpasuko wa chama hicho, uliotokana na kura za maoni, alisema anatarajiwa kukutana na wagombea wote walioshiriki katika mchakato wa kura za maoni na wapambe wao ili kuweka mambo sawa.
"Tayari nimefika Arusha kwa kazi hii moja kwanza kuunganisha makundi haya na pili kuzungumza ili tuweze kuanza kampeni za kuhakikisha tunashinda katika uchaguzi huu," alisema Nchemba
Nchemba ambaye pia alikuwa meneja kampeni wa chama hicho Jimbo la Igunga, alisema CCM ina uhakika wa ushindi katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
Wakati huohuo baadhi ya Wanachama wa CCM katika Kata ya USA River ambao wagombea waliokuwa wanawaunga mkono walishindwa na Sumari katika kura za maoni leo wanatarajia kujiunga na Chadema.
Akizungumzia suala hilo, Anaeli Mungure alisema hawajaridhiwa na uamuzi ya Kamati Kuu ya CCM, kumpitisha Siyoi kwani wanaamini hakupata kihalali nafasi hiyo.
"Sisi tunapinga uteuzi kwani haikuwa halali Sumari kupita, juzi tumepeleka ushahidi wetu Takukuru kwani vitendo vya rushwa vilitawala", alisema Mungure.
Alisema leo baadhi yao, wakiwamo pia baadhi ya viongozi wa UVCCM katika jimbo hilo, wanatarajia kujiunga na Chadema.
Bendera zawa kivutio
BENDERA za vyama vya CCM na Chadema zimeonekana kuwa kivutio kikubwa katika hekaheka za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki mkoani ambapo kwa sasa bendera hizo zimeonekana zikining”inia katika miti, milingoti, magari pamoja na kwenye paa za nyumba mbalimbali za wakazi wilayani humo.
Wilayani Arumeru kwa sasa mgeni akipita katika maeneo mbalimbali hususani pembezoni mwa barabara ya Moshi /Arusha watakutana na bendera za vyama hivyo viwili zikipepea hali ambayo imekuwa ni kivutio kwa wageni na wenyeji wilayani humo.
Wakati bendera za CCM zikionekana kuzagaa kwa wingi katika maeneo ya Tengeru na Usa River bendera za Chadema zimeonekana kuzagaa katika maeneo ya Maji ya Chai na Leganga ambapo madereva wa bodaboda waliopo Kituo cha Leganga wameonekana kuhamasika kuzitumia bendera za chama hicho.
Hata hivyo, wakati bendera hizo zikipepea wilayani humo tayari vyama hivyo viwili vimeanza kuwapa masharti makada wake kusimamia vyema bendera hizo kikamilifu kwa lengo la kuzilinda huku vikiwataka wale wote waliozembea hadi kusababisha bendera hizo kushushwa bila sababu za msingi kujieleza mbele ya chama.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza katika zoezi la kura za maoni ndani ya chama hicho zilizompatia ushindi Joshua Nassari alikaririwa akiwaamrisha makada wa chama hicho kuzining’iniza bendera za chama hicho kwenye nyumba zao na sio kwenye miti.
Dk Slaa alienda mbali zaidi na kuwaonya makada wote watakaozembea bendera zao kushushwa na wapinzani wao bila sababu za msingi wataitwa mbele ya vikao ili kujieleza ni kwa nini wameachia bendera hizo kushushwa.
Alisisitiza kwamba tayari uongozi wa chama hicho ngazi ya taifa unafanya jitihada za dhati kuhakikisha wanatuma bendera za kutosha ili ziletwe wilayani humo kwa lengo la kutumika.
Kwa upande wake, CCM mkoani Arusha kupitia kwa Katibu mwenezi wake, Loota Sanare alikataa kuzungumzia masuala ya bendera zao kwa madai kwamba masuala ya bendera ni mikakati ya siri ya chama chao na kamwe hawawezi kuitangaza hadharani mbele ya vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment