Matokeo ya utafiti mpya yaliyochapishwa katika jarida la
matibabu la Lancet, yamebainisha kuwa ugonjwa wa Malaria husababisha vifo vya
watu wengi duniani kuliko ilivyokisiwa.
Wanasayansi nchini Marekani na Australia wanasema watu milioni 1.2 waliaga
dunia mwaka wa 2010 kutokana na kuugua ugonjwa wa Malaria; idadi ambayo ni
asilimia 100 zaidi kuliko ilivyokadiriwa na shirika la umoja wa mataifa la afya
duniani WHO.
Wanasayansi hao wanasema zaidi ya asilimia 40 ya waliokufa ni watoto walio
na umri zaidi ya miaka mitano na watu wazima na hivyo kuhoji imani kuwa idadi
kubwa ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo huathiri watoto walio na umri wa
chini ya miaka mitano.
Watafiti hao wanasema takwimu hizo zimetokana na takwimu mpya na mbinu mpya
ya kuorodhesha vifo ambavyo hapo awali vilikisiwa kusababishwa na magonjwa
mengine.
Mhariri wa jarida hilo la Lancet, Richard Horton, aliiambia BBC kwamba
katika muongo mmoja uliopita, ni watu milioni 230 wametibiwa kutokana na
ugonjwa wa Malaria na idadi sawa ya vyandarua vilivyosambazwa kwa watu walio
katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.

No comments:
Post a Comment