Kiongozi wa zaman wa Boko Haram Mohamed Yusuf
Polisi nchini Nigeria wamemkamata msemaji wa kundi lenye
itikadi kali la Boko Haram ambalo limetekeleza mashambulio kadhaa hivi
karibuni.
Afisa wa polisi alisema jamaa huyo , anayejulikana kwa jina la bandia kama
Abul Qaqa, alikamatwa katika mji wa Maiduguri katika jimbo la Borno.
Afisa huyo aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba msemaji
huyo alikamatwa baada ya polisi kumfuatilia wakitumia simu yake.
Zaidi ya watu 150 waliuawa na kundi la Boko Haram mwezi uliopita; milipuko
kadhaa iliporomosha majengo ya polisi na ofisi za uhamiaji katika mji wa Kano.
Lilikuwa shambulio baya zaidi kuwahi kutekelezwa na kundi hilo.
Kundi hilo limesema linataka kupindua serikali ya Nigeria na badala yake
kuhakikisha nchi hiyo inatawaliwa kwa mujibu wa sheria za kiislamu.
Wanachama wa kundi hilo wameshambulia vituo vya polisi na majengo mengine ya
serikali na pia kulipua makanisa na kuwaua mamia ya watu wakiwemo Wakristo na
Waislamu.

No comments:
Post a Comment