Thursday, February 2, 2012

SI SAHIHI WASTAAFU KUPEWA MIKATABA



Waziri  Nchimbi .

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inakubali kuwa wastaafu kupewa mkataba wa kuendelea kufanya kazi si sahihi na kuahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi.
Akifanya majumuisho wakati wa mjadala wa Azimio la kuridhia mkataba wa vijana wa Afrika (The African Youth Charter) waziri Nchimbi alisema hatua ya wastaafu kupewa mikataba ya kuendelea na kazi inawanyima vijana haki ya kupata ajira katika taasisi mbalimbali.
Akizungumzia suala la maadili kwa vijana Mheshimiwa Nchimbi alisema hivi sasa vijana wakiwemo baadhi ya viongozi wanaotoa michango yao juu ya mambo mbalimbali katika mitandao kama vile facebook na twitter wanatumia lugha zisizojenga na badala yake aliwataka kutoa michango isiyokuwa na madhara kwa vijana wa taifa hili hasa ile inayotumia lugha zinazojenga ili kulinda maadili ya Mtanzania.
Aliwataka viongozi kuwa wa kwanza kupiga vita matumizi mabaya ya mitandao na kuacha tabia za kulipiza visasi pale wanapokosana na wenzao kwani hizo si sifa za kiongozi bora. “kiongozi bora na imara ni yule mwenye tabia ya kusamehe, alisema”.
Kuhusu mchakato wa kutafuta vazi la taifa waziri huyo alisema wizara yake inatekeleza maagizo yaliyotolewa na bunge na kuwaomba wabunge kuwa wa kwanza kuunga mkono wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inapotekeleza maagizo hayo. Aliongeza kuwa kamati iliyoteuliwa kutafuta vazi la taifa ni makini kwa kuwa imeundwa na watu makini waliotoka kwenye kada mbalimbali.
Awali akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM) Peter Serukamba alisema suala la wastaafu kupewa mkataba wa kuendelea na kazi halifai kwa kuwa linawanyima vijana haki yao ya kupata ajira. Alitoa mfano kuwa hivi sasa wenyeviti wa bodi wengi ni wastaafu ambapo ilipaswa nafasi hizo kuchukuliwa na vijana.

No comments: