Monday, February 27, 2012

NAHODHA DCI WASIGANA

ASEMA UCHUNGUZI BADO UNAENDELEA NA MATOKEO ATATANGAZA YEYE, ATAKA MANUMBA AULIZWE MWENYEWE CHANZO CHA TAARIFA YAKE
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema uchunguzi kuhusiana afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe bado unaendelea na ni yeye atakayetangaza matokeo ya kama alipewa sumu au la baada ya kukamilika huku akiikana ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kamishna, Robert Manumba.

Hii ni mara ya kwanza kwa Nahodha kutoa tamko hilo tangu kuibuka kwa mjadala kuhusu afya ya Dk Mwakyembe hasa baada ya DCI Manumba kuutangazia umma kwamba ripoti kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaonyesha kuwa Naibu Waziri huyo hakulishwa sumu, kauli ambayo ilipingwa na Waziri mwenye dhamana ya Afya, Dk Haji Mponda na Dk Mwakyembe mwenyewe.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Nahodha alisema uchunguzi kuhusu afya ya Dk Mwakyembe ni wa kisayansi na hauwezi kufanyika ndani ya wiki mbili au mwezi.

“Ninachosema ni kwamba uchunguzi nilioutangaza bado unaendelea,” alisema na kuongeza: Sasa mimi nimetangaza matokeo ya uchunguzi? Mimi ndiyo Waziri nasema uchunguzi bado unaendelea na mimi ndiyo nitatangaza hitimisho la jambo hilo.”

Alisema suala la Dk Mwakyembe ni zito na siyo la mtu kukurupuka kwani linagusa hisia za watu na kutahadharisha baadhi ya watu wanaojaribu kulifanya jepesi wanachezea kitu hatari.

“Ndiyo maana nasema ni jambo linalohitaji weledi wa hali ya juu katika kulichunguza. Ni jambo zito la kisayansi, naomba nipewe muda ili uchunguzi nilioagiza ufanyike kwa kina. Nasisitiza ni jambo linalohitaji weledi wa kisayansi.”

Waziri Nahodha alisema uchunguzi huo unafanyika kwa kuhusisha jopo la wataalamu wa sayansi hivyo kuwataka Watanzania kutambua kwamba uchunguzi huo unaendelea na ni vigumu kutamka utakamilika lini.

Kuhusu ripoti ya DCI   

Alipoulizwa ni kwa nini asimchukulie DCI Manumba hatua kwa kutoa tamko wakati uchunguzi alioagiza haujakamilika alisema: “Ndiyo maana nasema, uchunguzi wa suala hili unaendelea. Sasa hatima yote hayo unayozungumza nasema nipeni muda.”

Alipoulizwa ni wapi DCI Manumba alipata ripoti ya Dk Mwakyembe wakati mgonjwa mwenyewe na Waziri wa Afya wameikana, alijibu: “Sasa, hilo ni vyema ukamtafuta yeye mwenyewe DCI aseme. Mtafute aseme yeye na Waziri wa Afya, hao watu wawili wanaweza kuzungumzia ripoti hiyo, lakini mimi nasema uchunguzi wa jambo hili la Dk Mwakyembe ni wa kisayansi na bado unaendelea.”

Alisema alichokisema DCI Manumba kinaweza kuwa na msingi ambao anaujua mwenyewe hivyo, ni vyema akaulizwa yeye kuhusu undani wa ripoti yake huku akisisitiza: "Mimi ninavyoliangalia jambo hili la Dk Mwakyembe linahitaji umakini wa hali ya juu katika kulishughulikia. Hilo la DCI mtafute mwenyewe akueleze.”

Nahodha pia hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani hata pale alipoulizwa ikiwa haoni kwamba kukanwa kwa kiwango hicho kikubwa kwa ripoti ya DCI Manumba kunawafanya wananchi waanze kutilia shaka utendaji kazi wa jeshi la polisi.

Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusu kukanwa kwa ripoti yake na mawaziri, akiwemo wa Mambo ya Ndani ambayo ndiyo wizara mama inayosimamia Jeshi la Polisi, DCI Manumba alisema kimsingi hawezi kujibizana na waziri yeyote kwani kufanya hivyo itakuwa ni utovu wa nidhamu katika utumishi wa umma.

Alisema alichokifanya ni kuandaa jalada ambalo tayari liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye kwa mamlaka na utaalamu wake wa kisheria, ataamua cha kufanya baada ya kulipitia.

“Siwezi kujibizana na waziri wangu au waziri yeyote. Kama amesema uniulize mimi, ninachoweza kusema ni kwamba tayari nimeandaa jalada liko kwa DPP. Sasa nikianza kuzungumza hili au lile itakua haina maana watu watasema nimeanza kujitetea,” alisema.

DCI, Dk Mwakyembe na Dk Mponda

Akizungumza na waandishi wiki mbili zilizopita, DCI Manumba alisema: “Ukweli kuhusu kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo nayo imewasiliana na hospitali aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa zinaonyesha kuwa hakuna sumu.”

“Hatua zaidi zinachukuliwa dhidi ya jambo hilo, kwa sasa litashughulikiwa kwa kufuata misingi ya kisheria,” alisema Manumba.

Hata hivyo, siku moja baada ya kauli hiyo ya DCI Manumba, Dk Mwakyembe alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema: "Napata tabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa ‘nyingine’ na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au ‘walisomewa!’

“Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow (uboho) kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti au kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “Hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu.”

Dk Mwakyembe pia alitoa sababu kuu tatu za kupinga ripoti ya DCI Manumba: “Kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake, unaoendelea katika Hospitali ya Apollo, India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu, pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa ‘sikunyweshwa sumu’ wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.

Tatu ni kitendo cha Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima sasa, halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.

Januari 19, mwaka huu gazeti hili pia lilifanya mahojiano maalumu na Waziri Mponda ambaye naye alisema kwa utaratibu, ripoti ya daktari ni ya mgonjwa... “Sisi hatujaandika ripoti, muulizeni DCI Manumba awape ufafanuzi.”

Alisema wanaoweza kuzungumzia maradhi ya Dk Mwakyembe ni familia yake au yeye mwenyewe kwani ndiye mwenye ripoti. Lakini wizara haiwezi kufanya hivyo.




 MAGUFULI ACHIMBA MKWARA 

WAZIRI  wa Ujenzi, Dk John Magufuli ameipa siku saba kampuni ya ujenzi ya  Satos kutoka nchini Ufaransa, iwe imeanza kazi za awali za ujenzi wa barabara ya Arusha hadi Minjingu vinginevyo itakuwa imekosa sifa na atalazimika kuwakuza mara moja.

Mbali ya kutoa siku saba kwa mkandarasi huyo, Dk Magufuli pia amekataa mpango wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) mkoa wa Arusha, kutaka kuuza mitambo miwili ya kutengeneza barabara badala yake inapaswa karabatiwe ili itumike kwa ujenzi wa barabara na kukodishwa  kwa wakandarasi.

Dk Magufuli alitoa kauli hiyo juzi wakati akiweka jiwe la msingi la msingi katika majengo mawili ya makazi na biashara yenye ghorofa kumi kila moja katika mtaa wa  Wachaga na Wasukuma na jengo la makazi katika mtaa wa Simeon mjini Arusha kuwa  serikali haitavumilia kuona fedha ilizokopa zinachezewa.

“Nashangaa kuona hata hawajafanya mobilazition kwenye eneo waliloomba kazi,ninawapa siku saba,meneja wa Tanroad uwaambie wakishindwa kufanya kazi iliyowaleta nawatimua,tumekopa kiasi cha Sh.78 bilioni za watanzania wote kama hawezi nitamtimua hapa nchini,”alisema Magufuli

Alisema kwa sasa hapa nchini kuna Makandarasi wazawa wapatao 9000 katika madaraja tofauti hivyo hakuna haja ya kuendelea kuwabembeleza makandarasi wa kigeni wanachezea fedha za watanzania bila kutekeleza wajibu wao.

Magufuli aligeuka mbogo kwa TEMESA baada ya kuwaagiza kuacha mara moja mpango aliusikia wa kuuza mitambo miwili ya kujenga barabara na kuwa taka kuitengeneza ikodishwe katika shughuli za ujenzi.“Kwanini mnataka kuiuza?nyie si mnaitwa  mainjinia,nataka muitengeneze mara moja kama kuna vipuri mvitafute ili hiyo mitambi iweze kufanya kazi,”alisisitiza Magufuli

Kabla ya kuweka jiwe la msingi, alisema nchi nzima inakabiliwa na uhaba wa nyumba zipatazo milioni tatu na Wizara yake kupitia Wakala wa Majengo itaendelea kujenga nyumba kila mwaka na kuwa mwaka huu wa fedha imeshajenga zaidi ya nyumba 1043 katika mikoa mbalimbali.


Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la makazi duniani,inaonesha  wananchi kati ya asilimia 70 hadi 75 wanaishi katika makazi duni hivyo serikali itahakikisha inaboresha makazi  kulingana na uwezo wake.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Dk John Ndunguru, aliwataka TBA kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unakwenda kwa kasi na muda kama ilivyopangwa, huku akisisitiza weledi na uadilifu katika utekelezaji.

Mhandisi Dk Ndunguru alisema mradi huo ni muhimu kwa taifa hivyo, ni vema ukafanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha lengo la kubuniwa kwake linakamilika.


Awali, KaimuMtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo nchini(TBA), Elius Mwakalinga alisema wakala huo unahitaji kiasi cha Sh.5 bilioni ili kukamilisha ujenzi wa majengo hayo mawili yatakayopunguza uhaba wa nyumba mkoani Arusha kutokana na umuhimu katika utalii na mashirika ya kimataifa.





 WALIOTOKA CUF WAANZISHA CHAMA CHAO 
 ALIYEKUWA Meneja wa Kampeni za Urais wa CUF mwaka 2010, Said Miraji na wenzake jana waliwasilisha rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa maombi ya usajili wa muda wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Juzi, Miraji na aliyekuwa mgombea ubunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF, Adawi Limbu walijitoa chama hicho na kutangaza kusudio la kusajili chama kipya.

Jana, ujumbe wa chama hicho uliwasili katika Ofisi ya Msajili, Dar es Salaam saa 7:30 mchana ukiongozwa na Miraji ambaye alijitangaza kuwa ni Kaimu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake, Limbu na kupokewa na Wangalizi wa Ofisi ya Msajili, Galasia Simbachawene.

Akizungumza na viongozi hao, Simbachawene alisema  kulingana na taratibu za usajili wa vyama,  maombi ya chama kabla ya kuwasilishwa kwa msajili yanahitaji kupatiwa muda ili yapitiwe na maofisa mbalimbali akiwemo Mwanasheria wa Ofisi ya Msajili.

“Nimepokea maombi. Msiwe wasiwasi yameshafika kwa Msajili. Utaratibu uliopo ni kwamba maombi yanapokewa na kupewa muda zaidi wa kuyapitia kwa kushirikiana na mwanasheria ili kuona kama yamekamilika baada ya hapo yatawasilishwa rasmi kwa Msajili,” alisema Simbachawene.

Vitu vilivyowasilishwa jana ni barua ya maombi ya usajili, rasimu ya katiba ya chama iliyoambatanishwa na hati ya kwenda kwa msajili (PF1) pamoja na hati ya kiapo ya kuwa chama cha jamii chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya  mwaka 1992.

Miraji alisema wameamua kuanzisha chama hicho baada ya kutoona chama chochote cha siasa kinachowafaa  kujiunga akisema karibu vyote vinafanana tabia.

“Tumeamua kuanzisha chama cha siasa lakini, kitajikita kijamii zaidi.  Hatujafanya uamuzi wa kishabiki kwani siasa za nchi hii zilivyo, si rahisi mtu kutoka chama kimoja kwenda kingine kwani vyote vinafanana, vina maneno matamu sana hasa CCM ,” alisema Miraji.

Alisema ili kupata maoni ya wananchi kuhusu katiba ya chama hicho, rasimu ya katiba hiyo itaingizwa kwenye mitandao ya kompyuta pamoja na magazeti  na majarida na kusambazwa katika maeneo mbalimbali.
“Hatupo tayari kuwa na katiba ya mtu mmoja wala watu 100 tu, lazima tukusanye maoni ya muundo wa katiba kutoka kwa watu mbalimbali kupitia mitandao na kutoa matangazo kwenye magazeti yatakayoweza kuwafikia watu katika maeneo yote,” alisema Miraji.

Alisema katika katiba ya chama chao vitu walivyozingatia ni pamoja na ukomo wa madaraka na kuweka kamati maalumu ya usuluhishi ambayo haitawahusisha viongozi wa juu wa chama ili kuepeka kuwafukuza wanachama wanapofanya makosa ambayo yanaweza kurekebishika.

Kwa upande wake, Limbu alisema wananchi wanapaswa kuwa macho na vyama taasisi kwani viongozi wa vyama vya siasa wanafanya vyama hivyo kama mtaji.

“Chama hiki hakina mwenyewe watu wanaruhusiwa kuja kujiunga wasisubiri mpaka wafukuzwe katika vyama vingine ambavyo havijui umuhimu na thamani ya wanachama,” alisema Limbu.

Limbu aliwataka wanasiasa walio kwenye vyama visivyo na msimamo kuhamia chama hicho ili waweze kutetea haki za wananchi na kuwapa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Walikitabiria kifo CUF
Walipokuwa wakitangaza kujitoa CUF, Miraji na mwenzake walikitabiria kifo cha chama hicho wakisema kimepoteza mwelekeo kutokana na kuongozwa na watu wanaodhani ni mali yao.

Pia walimshutumu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro wakisema ameamua kwa makusudi kukiua.Hata hivyo, Mtatiro alijibu tuhuma hizo akisema, “Said Miraji ni mfuasi wa Hamad Rashid kwa muda mrefu sana.
Amekuwa akikihujumu chama yeye na Hamad Rashid, kuondoka kwake siyo tishio la CUF. Nafahamu anakwenda kukabidhiwa chama na Hamad Rashid kama kaimu mwenyekiti hadi Hamad atakamoliza ubunge wake, tunamtakia kila la heri katika kujitoa CUF.” 





 NOTI YA 5OO KUBADILSHWA KUWA SARAFU 

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeanza mchakato wa kufanyia mabadiliko ya noti mpya ya Sh500, ili iwe ya sarafu baada ya kujiridhisha kuwa inachakaa kwa haraka zaidi.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Arusha, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu, alisema mchakato kuifanyia mabadiliko na noti hiyo ili iwe katika sarafu, inazingatia ukweli  kwamba fedha iliyoko katika mzunguko mkubwa katika jamii.

Profesa Ndulu alisema noti ya Sh500  inatumika kwa kiasi kikubwa na wananchi wengi, jambo linalosababisha kuchakaa haraka kabla ya wakati uliopangwa.

“Tunafanya mchakato wa mabadiliko ya noti hizi zinazochakaa kwa haraka kwa sababu zenyewe zinatumika zaidi,” alisema Profesa Ndulu.

Alisema hatua hiyo haitaathiri mzunguko wa fedha na kwamba sarafu ya Sh500 itakapoanza kutumika, noti hiyo itaondoka polepole.

Alisema sarafu hiyo ya Sh 500 itaanza kupatikana  katika kipindi kifupi kijacho na kuwawezesha wananchi kuitumia.
 “Watanzania wasishituke mabadiliko hayo   ya noti za Sh500 kwenda sarafu maana hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kwa watoa chenji,”alisema. 

No comments: