Wednesday, February 8, 2012

NEC CCM

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (Nec), inatarajiwa kukutana kwa dharura mjini Dodoma Februari 12 mwaka huu.Kikao hicho cha Nec kinakuja kipindi ambacho upepo wa kisiasa ndani ya  chama hicho tawala umekuwa ukivuma vibaya, kufuatia wabunge wake kuingia katika vita ya chini chini na Serikali yao inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

Taarifa zilizopaatikana jana kutoka ndani ya CCM, zilisema tayari wajumbe wa Nec wamekwishafahamishwa kuwapo kwa kikao hicho cha dharura.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, pamoja na mambo mengine, kikao hicho cha Nec kitajadili masuala ya mchakato wa Katiba ya chama hicho.

Taarifa hizo zilifafanua zaidi kwamba, wajumbe watajadili jinsi ya kuwapata wajumbe wa Nec upande wa Zanzibar, baada ya katiba ya chama hicho kufanyiwa marekebisho kuhusu taratibu za kuwapata wajumbe hao.

Kauli Nape

 
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye  alithibitisha kuwapo kwa kikao hicho cha Nec na vingine vya chama hicho tawala lakini, akisema si vya dharura.

Nape alisema leo kutakuwa na kikao cha Sekretarieti ya chama hicho itakayokutana mjini Dodoma.
Kamati ya Maadili

Alitoa ratiba ya vikao hivyo akisema, Februari ya 11 mwaka huu kutakuwa na kikao cha Kamati ya Maadili asubuhi na kufuatiwa na kikao cha Kamati Kuu (CC) baadaye mchana.

Katibu huyo aliongeza kwamba, Febrauri 12 kutakuwa na kikao cha Nec huku ajenda kuu ikiwa ni kupitia mabadiliko ya katiba ya chama ili kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi.

"Tunafanya hivyo kwakuwa kuna watu walikuwa wanahoji uchaguzi
utafanyikaje wakati Nec haijakaa, kwa hiyo hiki ni kikao maalumu cha mabadiliko ya katiba ili uchaguzi ufanyike, " alisema Nape.

CCM imeanza mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa ndani ya chama hicho ambao uchukuaji wake wa fomu ulianza Februari 4 mwaka huu huku uchaguzi ukitarajiwa kuendelea awamu kwa awamu, kuanzia jumuiya na chama hadi Juni.

Vikao hivyo vya juu vya chama vinafanyika wakati pia chama hicho kikiwa bado hakijatekeleza mpango wa kujivua gamba ambao kwa sasa ulirudishwa CC kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.

No comments: