Saturday, February 4, 2012

WAZIRI APIGWA MAWE





 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, juzi alionja 'joto ya jiwe' baada ya msafara wake kupigwa mawe alipokuwa kwenye ziara ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya.Tukio hilo la tatu kwa viongozi wa Serikali kushambuliwa mkoani Mbeya, lilitokea eneo la Soko la Tunduma (Kisimani), wilayani Tunduma.

Habari zilieleza kuwa tukio hillo lilitokea wakati Waziri huyo na msafara wake walikuwa wanapita kuelekea ofisi za CCM Kata ya Tunduma ambako alitakiwa kufanya mkutano wa hadhara.


Ilikuaje?


Dalili za machafuko zilianza wakati msafara huo unapita kwa baadhi ya vijana wanaofanya biashara ya kubadilisha fedha sokoni hapo kuanza kujipanga barabarani wakizomea na kupiga miluzi.


Wengi wa vijana hao walisikika wakilaumu kitendo cha Waziri huyo wa Mambo ya Ndani kutumia magari ya Serikali katika msafari wake wa kichama.


"Haya ni matumizi mabaya ya mali za umma," alisikika akisema mmoja wa vijana hao.


Vijana hao walianza kumzomea waziri huyo huku baadhi wakirusha mawe kabla ya kudhibitiwa na polisi waliokuwa wanasaidiana na walinzi wa CCM maarufu kwa jina la Green Guard.


Katika sekeseke hilo vijana wawili walikamatwa na kukabidhiwa katika Kituo cha Polisi cha Tunduma.

 
Hata hivyo, Mkuu wa kituo hicho ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa yeye sio msemaji wa polisi, alikiri kuwapokea vijana hao na kueleza kuwa wanaendelea kuwafanyia mahojiano.

Mmoja wa vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Yusuf Haonga alisema wamechukua hatua hiyo kwa vile Waziri huyo aliwachanganya kwa kutumia magari ya Serikali akiwa kwenye ziara ya chama.


“Hawa wanatuchanganya, inakuwaje wanatumia rasilimali za nchi kwa kazi za chama. Pesa hizo si zingetumika kuhudumia wagonjwa waliolala mahosipitalini badala yake wanazitumia wao,”alisema Haonga.

Haonga alisema kuwa kitendo cha Waziri akiwa mtumishi wa umma kufanya ziara ya kichama kwa magari ya Serikali, kiliwakera na waliamua kumtupia mawe ili kutoa onyo kwa viongozi wengine wa Seriakali.

Hata hivyo, habari zingine zilieleza kuwa vijana waliomrushia mawe Waziri huyo ni wafuasi wa Chadema.


Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vijana wakiwa na bendera za chama hicho cha upinzani ambao pia walikuwapo kwenye msafara huo uliomalizikia kwenye mkutano huo wa hadhara.


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alipopulizwa kuhusu tukio hilo alihoji "Unataka niseme nini? Mimi niko Dar es Salaam na tukio hilo limefanyika Mbeya."


Aliendelea, "Ndio kwanza unaniambia (mwandishi). Inabidi nijue nini kilitokea na kama kweli ni vijana wa Chadema nijue walikasirishwa na nini."


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu," Sina taarifa."


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo, Abbas Kandoro jana alishindwa kuzungumzia tukio hilo kwa kile alichoeleza kuwa yuko kwenye safari ya kikazi jijini Dar es Salaam.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliohutubiwa na Nahodha, mwenyekiti wa CCM Kata ya Tunduma, Daniel Mwashiuya alisema kuna kikundi cha watu ambacho kimeanza kupoteza amani ya mji wa Tunduma kutekeleza matakwa yao ya kisiasa.

Alisema “mazingira tunayokwenda nayo kwa sasa si mazuri kwa ustawi wa mji wetu hivyo Wanatunduma tujiepushe na kuvunja amani tuliyoizoea ili isije ikapotea,” alisema


Kauli ya Waziri Nahodha

Akihutubia mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo, Waziri Nahodha alisema hajapendezwa tukio hilo na kuhoji, "Kama limefanyika kwangu hali ikoje kwa watu wengine?"


Alisema kamwe hawezi kuacha hali hiyo ya uvunjifu wa amani iendelee na kuiagiza polisi mkoani Mbeya kuchukua hatua haraka dhidi ya kikundi hicho cha watu aliowaita wahuni.


Waziri Nahodha pia amepiga marufuku biashara haramu ya kubadilisha fedha katika eneo hilo.


Alisema mtu anayetaka kuendelea kufanya kazi hiyo itabidi afuate taratibu zinazotakiwa ili aweze kuihalalisha biashara yake.


“Sokoni pana biashara za aina mbalimbali zilizo halali na haramu, lakini nawaagiza polisi chini ya Kamanda wenu wa Mkoa, mkae muangalie namna ya kurejesha amani mahali hapo. Sasa likizo basi,” alisema Nahodha.

Waziri Nahodha alisikitishwa na taarifa za kuendelea kuvunjika kwa amani katika mji wa Tunduma ambapo aliwataka wananchi wa mji huu kuthamini amani iliyojengeka kwa muda mrefu.

Aliwataka wasidhani kwamba amani iliyopo imeshuka kutoka Mbunguni na kwa sababu hiyo wao wenyewe wailinde na kuidumisha kwa kushirikiana na polisi kwa njia ya ulinzi shirikishi.


Historia ya matukio


Hili ni tukio la tatu kwa viongozi wa kitaifa kuzomewa katika mji wa Tunduma ambapo mwaka 2010, mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, alizomewa katika eneo hilo alipokuwa akipita kutokea mkoani Rukwa katika ziara za kampeni za uchaguzi.


Mwaka 2009, Mwenge wa Uhuru ulilazimika kubadili njia ghafla kufuatia dalilili za uvunjifu wa amani.


Tukio jingine ilikuwa ni Oktoba, 2008, ambapo msafara wa Rais Jakaya Kikwete kushambuliwa kwa mawe kwenye kijiji cha Kanga, wilayani Chunya.


Tukio hilo lilitokea katika Kijiji hicho wakati msafara wa Rais ukiwa njiani kuelekea Mbeya mjini ukitokea mji wa Mwakwajuni wilayani Chunya ambako alikuwa amefanya ziara.

Kwa mujibu wa habari hizo magari sita yaliyokuwa kwenye msafara huo yalishambuliwa kwa mawe na baadaye vijana kadhaa walikamatwa.

Ilidaiwa kuwa waliofanya tukio walikuwa wamejipanga pembeni mwa barabara na baada ya magari manne ya mwanzo kupita, likiwamo la Rais Kikwete, ndipo mawe yalianza kuvurumishwa.


Hata hivyo, ilidaiwa kuwa wananchi hao walikasirishwa na  kitendo cha kushindwa kumwona Rais Kikwete baada ya kumsubiri kwa muda mrefu ili awahutubia na kusikiliza kero zao.

 
 
 
......................................................................................................................................
 
 
 
 
 WAMTAKA WAZIRI WA AFYA AJIUZULU.
 
 
 KAMATI ya wabunge wa CCM imemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, Naibu wake, Dk Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, kujiuzulu kwa kile walichoeleza kuwa wao ni chanzo cha mgomo wa madaktari unaendelea nchini.Wakati hayo yakijitokeza, Bunge limejitosa kusuluhisha mgogoro huo kwa kusikiliza pande zote zinazohusika; Serikali na madaktari.

Pia, wabunge hao wa CCM wanadaiwa kuishutumu Serikali kwa kuchukua muda mrefu kabla ya kuingilia kati masuala muhimu ya taifa likiwamo hili la mgomo.Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika juzi usiku, zimeeleza kuwa wabunge hao walidai kuwa viongozi hao wamekuwa kiini cha mgogoro wa madaktari kwa kushindwa kutoa suluhisho na kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.


Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), anadaiwa kuwa wa kwanza kutaka viongozi hao wajiuzulu na wakikaidi wawajibishwe na mamlaka husika yani Rais.


Pendekezo hilo liliungwa mkono na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliyehoji hatua ya Serikali kuchelewa kutoa uamuzi kuhusu masuala ya kitaifa.Sendeka anadaiwa alituhumu Serikali kushindwa kuingilia kati haraka migogoro inayojitokeza nchini na kusubiri hadi maafa yatokee.


Kauli ya Serikali bungeni

Akiwasilisha kauli ya Serikali bungeni jana, Dk Mponda huku akitoa mlolongo wa historia ya mgomo huo, alisema Januari 30, mwaka huu, Serikali iliunda kamati ya kushughulikia maazimio yaliyowasilishwa na madaktari kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Dk Mponda alisema kamati hiyo itayachambua na kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia Serikali kumaliza mgogoro huo wa watumishi wa sekta ya afya na kwamba, tayari imeanza kazi.


“Kamati hiyo inajumuisha wajumbe kutoka Ofisi ya Rais (Utumishi), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Fedha, Tughe, mwakilishi wa madaktari, mwakilishi wa wauguzi, Tamisemi, Mwanasheria Mkuu na Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Ajira,” alisema.Waziri Mponda alisema kamati hiyo imepewa hadidu za rejea zinazoainisha masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi na itafanya kazi kwa wiki mbili.


Hadidu za rejea zilizotolewa ni kupitia hali ya sasa ya maslahi ya madaktari na watumishi wengine wa kada za afya; kupitia, kufanya uchambuzi wa kina wa madai ya madaktari na watumishi wengine wa kada hiyo; kubaini gharama za utekelezaji wa madai ya maslahi ya madaktari na watumishi wengine wa sekta hiyo.


Nyingine ni kupendekeza na kushauri namna bora ya kushughulikia madai ya watumishi hao kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu na kuandaa taarifa na kuiwasilisha kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.


Awali, Dk Mponda alisisitiza kuwa mgomo huo siyo halali kwa sababu kisheria madaktari hawaruhusiwi kugoma.

“Masharti haya yanaainishwa katika kifungu cha 77 (1)(a) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano kazini (Na.6 ya mwaka 2004) ambayo inazuia kugoma watumishi wote walio katika ‘huduma muhimu’ (Necessary Services),” alisema.
Dk Mponda alisema madaktari wapya wanaoajiriwa wanalipwa 957,700, huku watumishi wa kada nyingine kama wahandisi wanaanza na Sh600,000 na wahasibu wanaanza na mshahara wa Sh469,200.

Alisema utekelezaji wa pendekezo la madaktari la kulipwa mshahara wa Sh3.5 milioni kwa mwezi kwa daktari atakayeanza kazi, utalazimu Serikali kurekebisha viwango vya mishahara kwa watumishi wote wa afya na kada zingine na mhudumu wa sekta hiyo atakuwa analipwa Sh670,316 na mshahara wa juu wa kada hiyo utakuwa Sh8,145,573.

“Utekelezaji wa pendekezo hili utaigharimu Serikali Sh83,508,834,430 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh417,544,172,150 kwa kipindi kilichobaki cha miezi mitano mwaka huu wa fedha,” alisema.

Hata hivyo, Dk Mponda alisema hivi sasa hali ni nzuri isipokuwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), ambako alidai wanawasiliana na Wizara ya Ulinzi na JKT kwa ajili ya kupeleka madaktari wanajeshi.


Kauli za wabunge

Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisimama na kutumia kanuni ya 53 (a) ambayo inatoa ruhusu ya kutengua kanuni yoyote, huku akitaka kutengeuliwa kwa kanuni 49 (2) inayozuia kauli inayopelekwa na Serikali kujadiliwa bungeni.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), aliyesema kauli hiyo ni muhimu sana, inayohusu afya za Watanzania na sekta ambayo inatengewa fedha nyingi lazima ijadiliwe.

Awali, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), akitumia kanuni ya 5 (1) na Ibara ya 63 (2), alitaka kanuni ya 49 (2) kutenguliwa kutokana na unyeti wa kauli hiyo.

“Serikali ni mmoja wa watuhumiwa kutokana na waziri, naibu wake na katibu mkuu kwa utendaji wao mbovu …itapelekea tushindwe kuijadili na tusiwawajibishe kwa ubovu wao,” alisema Mnyika.


Kauli ya Naibu Spika

Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema hoja hizo hazikuungwa mkono na wabunge kwa hiyo wanabanwa na kanuni zao, huku akiwataka watakapokuwa wazinafanya marekebisho kuangalia kanuni hiyo.

Hata hivyo, Ndugai alisema suala la mgomo wa madaktari ni zito na kwamba, tatizo lililojitokeza ni kusikiliza upande mmoja wa Serikali kwa sababu, madaktari hawawezi kwenda kusimama bungeni kueleza madai yao.


“Waziri ametueleza kuwa wameunda kamati ya kupitia madai ya madaktari,  nakumbuka mojawapo ya madai yao ambayo Serikali haikutaja hapa na hiyo nina uhakika hiyo kamati haitasema ni kwamba, Wizara ya afya kuna baadhi ya watendaji wenye uwezo wa kiutendaji wana kauli mbaya na dharau,” alisema Ndugai na kuongeza:


“Hiyo haimo. Uamuzi wa kuhusu jambo hili nalipeleka Kamati ya Huduma za Jamii, ilifanyie kazi haraka kwa kuita pande zote zinazohusika ziweze kueleza madai yao na tutapata mwafaka haraka.”

 
 
 
 
 
......................................................................................................................................
 
 
 
 
 
HAMAD RASHID AZUIWA KUFANYA MKUTANO
 
 
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limezuia mkutano wa mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed kwa kile ilichodai kuwa mbunge huyo hatambuliwi na chama chake.

 Mkutano huo uliokuwa ufanyike leo katika Wilaya ya Handeni eneo la soko la zamani Chanika, ulikuwa  na lengo la kwenda kuwaeleza sababu za kufukuzwa uanachama katika chama cha CUF.
Akizungumza na gazeti hili  kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tanga, Constatine Massawe alisema kuwa wameshindwa kutoa kibali cha kufanya mkutano huo kutokana na kupata barua ya kutowatambua wanachama  hao kutoka katika ofisi kuu ya chama cha CUF.

“Hakuna kibali cha mkutano wa wanachama wa CUF kilichotolewa kwa sababu tumepata barua kutoka ofisi ya chama iliyoletwa na mwenyekiti  kwamba wamemvua  uanachama huyo kiongozi anayetaka kufanya mkutano,” alisema Massare. Alisema kutokana na hali hiyo hawataweza kuruhusu kufanyika kwa mkutano kwani tayari kunaonyesha kuwa na tofauti kati ya pande hizo mbili ambazo zinaweza zikasababisha vurugu.

Alisema aliongea na mkuu kituo wa kituo cha polisi Handeni awatafute viongozi hao na aongee nao wakipata suluhu wanaweza wakaendelea na mkutano huo.

Awali Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni, Seth Mwakajinga ambaye yeye alisema si msemaji alieleza   kuwa ameshindwa kutoa kibali kwa sababu ya ugomvi uliopo kwani katibu anasema hatambui uongozi huo unaotaka kufanya mkutano.
“Barua yao ilikuwa na maombi matatu ambapo waliomba mikutano miwili na kikao cha ndani kimoja nimezuia vyote mpaka watakapokaa wenyewe na kuelewana na kupata suluhu juu ya ugomvi wao,” alisema Mwakajinga.
Alisema wameshindwa kuruhusu mkutano huo kwa kuhofia kutokea vurugu na kwamba hataweza kuruhusu mkutano huo mpaka wahusika watakapokaa na kuongea vizuri na kukubaliana.

Hivi karibuni mbunge huyo pamoja na wenzake 13 waliingia katika mgogoro jambo lilosababisha kufukuzwa uanachama katika mkutanao wa Baraza Kuu la CUF uliofanyika mwanzoni mwa mwaka huu visiwani Zanzibar.
Tangu kutokea kwa sakata hilo mbunge huyo amekuwa akizunguka katika maeneo mbalimbali na kuwaeleza wanachama sababu ya kuvuliwa uanachama wake.

Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo Hamad alikwenda kuweka pingamizi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa amri ya kuzuia mkutano huo lakini uliendelea kufanyika.

Mara baada ya maamuzi hayo, Hamad alifungua kesi mahakama Kuu kupinga maamuzi hayo na kesi hiyo bado inaendelea kusikilizwa.Hata hivyo ofisi ya Bunge ilisema bado inamtambua Hamad kama mbunge kupitia chama chake cha CUF. 

Source;Mwananchi.

No comments: