
Hivi karibuni mchawi wa soka duniani Pele alitimiza umri wa miaka 70 akiwa
bado mwenye nguvu na afya njema. Alisifika enzi zake kwa uwezo wake mkubwa wa
upigaji chenga, kutoa vyumba safi kwa wafungaji wenzake, kufunga kwa vichwa
mithili ya mpira uliopigwa kwa mguu na alikuwa na nguvu ya miguu. Huyo ni pele
aliyeanza kuichezea timu ya taifa ya Brazil katika Kombe la Dunia akiwa na umri
wa miaka 17 mwaka 1958.
Msakata kandanda mwengine hodari kuwahi kutokea duniani ni Diego Maradona
anayefikisha umri wa miaka 50. Akiichezea timu yake ya taifa ya Argentina
alikuwa chachu ya ushindi kwa kikosi kikali cha nchi hiyo katika Kombe la
Dunia. Hivi sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Argentina, ambapo alishindwa
kuipelekea Kombe la Dunia nchi yake wakati wa mashindano ya Afrika Kusini mwaka
2010.
Wapenzi wa soka duniani kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka kumaliza ubishi
kati ya wanasoka hawa wawili bora zaidi duniani, nani alikuwa zaidi ya
mwenzake?
Fifa iliwahi kuchapisha kura ya kumtafuta mchezaji bora wa soka wa karne,
lakini hawakufurahishwa baada ya matokeo kuonesha Maradona ndiye
aliyeshinda.
Kwako mpenzi wa soka uliye mkereketwa hata kama hukuwahi kuwashuhudia
wakisakata soka enzi zao, unadhani kati ya wawili hawa, Pele na Maradona nani
alikuwa zaidi? Ni mjadala wa siku nyingi lakini si vibaya tukiuamsha upya
wakati wachawi hawa wa soka wakiwa wnasherehekea siku zao za kuzaliwa.

No comments:
Post a Comment