TANZIA
CHADEMA YAPATA PIGO
TANZIA!
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimepatwa na majonzi makubwa na kinasikitika sana kwa kifo cha Mjumbe wa Kamati
Kuu ya Chama Taifa, Mheshimiwa Regia Mtema ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum
na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira. Mheshimiwa Regia Mtema amefariki leo tarehe
14 Januari 2011 kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu darajani.
Katika uhai wake marehemu Regia Mtema amefanya kazi
mbalimbali za kisiasa na kijamii katika taifa. Marehemu Regia Mtema amezaliwa
tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 1980 na kusoma shule za sekondari kidato cha
kwanza mpaka cha sita katika shule ya sekondari ya Forodhani na Shule ya
Wasichana ya Sekondari ya Machame. Marehemu Regia Mtema alipata shahada yake ya
kwanza (Bsc Home Economics and Human Nutrition) katika Chuo Kikuu cha Kilimo
cha Sokoi
ne.
Mara baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia
Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na
kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na
baadaye kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA
nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti
maalum.
Viongozi wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti
Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Katibu
Mkuu Dr. Wilbroad Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa chama makao makuu
na wabunge wamejumuika hivi sasa na familia ya marehemu katika kipindi hiki
kigumu.
CHADEMA inatoa pole kwa familia ya marehemu Regia
Mtema, wanachama wote na wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wa Jimbo la
Kilombero kutokana na msiba huu wa ghafla katika wakati ambapo mchango wake
ukihitajika kwa chama na kwa taifa.
Taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa
mara baada ya kukamilisha majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na
Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mipango ya mazishi ya marehemu inapangwa nyumbani
kwa Baba wa Marehemu Regia Mtema, Ndugu Estelatus Mtema, Tabata Chang'ombe.
Ratiba ya maziko itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazopangwa na
familia ya marehemu, Ofisi ya Bunge na chama.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia Mtema, mahali
pema peponi. Amina.
Imetolewa na:
John Mnyika(Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment