Polisi Mkoani Ruvuma, wanawashikilia na kuwahoji askari wake wanne kwa tuhuma za mauaji ya raia kwa kutumia risasi za moto katika vurugu zilizotokea juzi mjini Songea.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda alisema jana kuwa askari hao walikamatwa na wanaendelea kuhojiwa ili kujua kama kulikuwa na uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao.“Kwa kuwa tukio hilo limehusisha vifo, hatuwezi kuacha hivihivi tu ni lazima tujiridhishe kuwa askari hao hawakufyatua risasi kwa uzembe,”alisema Kamhanda.
Kamanda huyo alisema askari hao watahojiwa baada ya kuundwa kwa tume maalumu ya kuchunguza tukio hilo, na tume hiyo ikibaini kuwa kulikuwa na uzembe, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo kamanda Kamhanda hakutaka kutaja majina, wala vyeo vya askari hao kwa maelezo kwamba ni ni mapema mno, pia sababu za kiusalama.Katika hatua nyingine Kamhanda alisema tayari watu 54 wamefikishwa mahakamani kutokana na vurugu za juzi.
IGP Mwema achunguza
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema ametuma kikosi cha maofisa waandamizi kutoka makao makuu ya jeshi hilo, kikiongozwa na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja kwenda mjini Songea kufanya uchunguzi wa ghasia hizo.
Chagonja akizungumza na Mwananchi jana alisema maandamano hayo hayakuwa ya amani bali ya kihuni kwani yalilenga kuvamia ofisi za serikali ikiwemo Ikulu ndogo na Ofisi ya Mkuu wa mkoa. Chagonja alikuwa akijibu swali lililotaka aeleze endapo haoni kama polisi imetumia nguvu kubwa kutawanya raia waliokuwa wakiandamana kwa amani.
"Maandamano ya amani watu wanavamia Ikulu, maandamano ya amani watu wanazingira ofisi ya mkuu wa mkoa?"
"Sijafika huko ndo naelekea lakini, yale si maandamano ya amani. Yaani wahuni wanataka kuivuruga nchi waachiwe? Kuweni wazalendo, msiwe kama labda ninyi ni waandishi wa BBC kutoka Uingereza, hii ni nchi yenu."
Alifafanua kwamba, maandamano ya amani yanafahamika kwani watu hulazimika kuomba kibali na kuweka wazi ajenda ya maandamano "Lakini siyo maandamano yale, watu hayakuwa na kibali chochote, wahuni wamejiingiza wanataka kuvuruga nchi tu."
Mkuu huyo wa operesheni alitetea polisi akisema,"Usifikirie polisi hawana akili. Haiwezekani watu wazima na akili zao wenye mafunzo wafyatue hovyo risasi za moto kwa raia. Hakuna askari anapenda kuua raia..., lakini watu wanavamia Ikulu, ofisi ya mkuu wa mkoa, magari ya polisi hapo kuna amani kweli?"
Alitoa angalizo kwamba ni lazima hata vyombo vya habari, viache ushabiki badala yake viangalie maslahi ya taifa kwani nchi ikivurugika wao pia hawatasalimika na kusisitiza, "Kuweni wazalendo bwana, msifikirie kulishutumu jeshi la polisi tu."
Wakati IGP akituma kikosi hicho, wanaharakati, wanasiasa na wasomi wamekosoa matumizi makubwa ya nguvu za polisi dhidi ya raia na waandamanaji waliokuwa wakifikisha ujumbe wao kwa mkuu wa mkoa kupinga mauaji ya watu tisa yaliyofanywa kwa imani za ushirikina.
Juzi wananchi waliokuwa wakiandama kupinga mauaji hayo, walipambana na polisi ambapo watu wanne waliuawa na wengine 41 kujeruhiwa.
Hali za majeruhi Majeruhi wanane kati ya 11 waliolazwa katika Hospitali ya mkoa wa Ruvuma, jana waliruhusiwa. Majeruhi wengine 30 walipatiwa matibabu juzi na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza alisema tayari wagonjwa wanane kati ya kumi na moja waliolazwa katika hospitali hiyo wameruhusiwa na kwamba ni wagonjwa watutu ndio waliobaki.
Mmoja wa wagonjwa hao, Shangwe Mtaula (16) mkazi wa Mabatini hadi jana alikuwa hajitambui kutokana na kipigo cha polisi kilichosababisha kuumia vibaya katika paji lake la uso.
Muuguzi wa wodi alimolazwa mgonjwa huyo, Hildetha Mhonyo alisema binti huyo alifikishwa hospitalini hapo juzi saa tano asubuhi akiwa hajitambui na hivyo alilazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi.
Muuguzi huyo alisema, bado hali ya Shangwe si nzuri ingawa jana alianza kuzungumza kwa taabu na kwamba anaonekana kuwa na maumivu makali kwenye paji lake la uso, huku macho yake yaonekana kuvimba.Mgonjwa mwingine ni Esta Mbali (29) mkazi wa Mshangano, ambaye amelazwa wodi namba tano baada ya kupigwa risasi katika bega lake la kushoto na kuumizwa vibaya.
Mgonjwa huyo anasema, hali yake inaendelea vizuri kwa sasa baada ya kupata matibabu. Alisema, katu hatasahau tukio hilo kwani alikuwa akitoka hospiatali kumsalimia binamu yake ambaye alikuwa amejifungua na wakati akiwa njiani alikutana na kundi kubwa la watu wakiandamana na baadaye polisi walianza kuwatawanya kwa mabomu ya machozi, ambapo alifanikiwa kukimbia na kujificha kwenye nguzo ya umeme, lakini ghafla alisikia kitu cha moto kikimuumiza begani mwake . Alisema alipatwa na kiwewe na kuanza kukimbia ovyo, hali iliyosababisha mwili mzima kulowa kwa damu ambayo wakati huo hakuweza kufahamu chanzo chake.
Esther aliendelea kusimulia kuwa baada ya kutokwa damu nyingi, aliishiwa nguvu na kuanguka, hadi aliposaidiwa na wasamaria wema ambao walimpakia kwenye gari na kumkimbiza hospitalini.
Mwingine ni Sinje Mchompa (29) mkazi wa Bombambili, ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo na kuumizwa vibaya na kipande cha bomu mdomoni eneo la SODECO, wakati alipokuwa akielekea Mabatini.
Sinje alisema alipokuwa katika eneo hilo ndipo vurugu zilianza na kwamba alishtukia akipigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni kipande cha bomu mdomoni na kutoboka mdomo hali iliyosababisha meno kuuma sana.
Mgonjwa huyo ameomba msaada wa kupatiwa matibabu zaidi ili hali yake iweze kurejea kama awali.
Kwa upande wake Matroni wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma Helta Soko, ametoa ushauri kwa wananchi kuacha tabia ya kufanya vurugu katika maeneo ya hospitalini kwani hali hiyo inasababisha usumbufu kwa wagonjwa waliolazwa.
Kauli ya Helta inatokana na baadhi ya wananchi kupiga kelele wakati walipokuwa wakiwarushia mawe wauguzi na askari waliokuwa wakipeleka mwili wa mmoja wa waliokufa katika tukio hilo katika chumba cha maiti.
Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, kwa mara nyingine, jana saa 12 jioni, polisi mjini Songea walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwaokoa watu wawili waliokuwa wakipigwa na wananchi wakiwatuhumu kwamba ni majambazi wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya wananchi.
Watu hao ambao walijeruhiwa vibaya walikamatwa na wananchi katika eneo la Mkuzo nje kidogo ya Manispaa ya Songea baada ya kujitambulisha kwa wenyeji kwamba wao walikuwa wakitatafuta shamba la kununua, huku mmoja wao ambaye ni mwanamke akitoroka na kukimbilia kusikojulikana.
Kutokana na kuwatilia mashaka, wananchi hao waliwazingira na kuwaweka chini ya ulinzi kisha kuwafikisha nyumbani kwa kiongozi wa Serikali ya mtaa wa Mkuzo, John Moyo na baadaye walianza kuwapiga baada ya kutokea utata katika maelezo yao.
Kuona hivyo moyo alipiga simu polisi ambao walifika na kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi, hivyo kuwaokoa watuhumiwa hao kisha kuwakimbiza katika hosipitali ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matibabu.
Watuhumiwa hao ambao wametambuliwa kwa majina ya Gervase na Juma, walikuwa wakivuja damu katika sehemu kadhaa za miili yao na polisi walipowafanyia upekuzi waliwakuta wakiwa na hirizi na nyaraka zilizoandikwa kwa lugha ambayo haikuwa rahisi kusomeka.
NAHODHA JELA MIAKA 20 KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI
Jaji Agustine Mwarija alitoa hukumu hiyo jana na kuwatia hatiani washitakiwa hao ambao ni nahodha wa meli hiyo Husu Chin Tai na wakala wa meli hiyo Zhao Hanquing lakini, akiwachia huru washitakiwa wengine watatu.
Nahodha Tai ambaye ni mshitakiwa wa kwanza alihukumiwa adhabu mbili kwa pamoja ambazo ni kwenda jela miaka hiyo 20 au kulipa faini ya Sh 1bilioni na kosa la pili, kutumikia kifungo cha miaka 10 au kulipa faini ya Sh 20bilioni.
Adhabu kama hiyo pia ilitolewa kwa mshtakiwa wa saba, Zhao Hanquing na adhabu zote zinakwenda pamoja.
Mashitaka
Washtakiwa wote watano walikuwa wakikabiliwa na makosa mawili
kwa pamoja, la kwanza likiwa ni kufanya shughuli za uvuvi katika ukanda huo wa Tanzania bila kibali na kuchafua mazingira ya bahari kwa kumwaga mafuta na uchafu wa samaki majini.
Lakini, mshtakiwa wa saba Hanquing na mshtakiwa wa tisa Sheng Pao wao walikuwa wakikabiliwa na kosa jingine la kujaribu kuwaepusha wenzao na adhabu kutokana na makosa waliyokuwa wakituhumiwa .
Walioachiwa huru katika kesi hiyo ni wahandisi wawili wa meli hiyo, Cai Dong Li ambaye alikuwa mshitakiwa wa 33, Cheng Rui Hai wa 34; na mshitakiwa wa tisa, Hsu Sheng Pao kutokana na kile Jaji Mwarija alichosema ni ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma zao.
Kuhusu washtakiwa wa 33 na 34, Jaji Mwarija alisema watuhumiwa hao walikuwa na jukumu la kuhakikisha usalama wa meli tu kwani
wakiwa wahandisi hawakuwa na nafasi ya kujua masuala ya leseni wala mahali walipokuwa wakivua na kwamba majukumu hayo ni ya Nahodha na wakala.
Kuhusu mahali walikokuwa wakivua kama ni Ukanda wa Kiuchumi wa Tanzania au la, Jaji Mwarija alisema hilo ni jukumu la nahodha, huku akizingatia utetezi wa washtakiwa hao kuwa hawajui hata kusoma ramani.
Akimzungumzia mshtakiwa wa tisa, Pao, Jaji Mwarija alisema hana hatia kwani hakuwamo melini.
Jaji Mwarija alisema mbali na kitendo chake cha kuambatana na mshtakiwa wa saba (Hanquing), hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa mahakamani hapo unaothibitisha makosa aliyofanya.
Jaji Mwarija alisema ameridhika na ushahidi wa mazingira uliotolewa na upande wa mashtaka akiwemo shahidi wa tatu, Nahodha Ernest Bupamba ambaye ni Msimamizi wa Shughuli za Uvuvi na Sheria za Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, ambaye pia ndiye aliyewakamata washtakiwa hao, akiwa na wanadoria wenzake wa mataifa mengine matano ya Afrika.
Jaji Mwarija aliuelezea ushahidi huo wa mazingira kuwa ni pamoja na kukutwa na samaki, ambao walikuwa hawajaganda kwenye friji na kufungwa kwa madirisha madogo ya kutolea maji kwenye meli (Scuppers).
Bupamba katika ushahidi wake, aliieleza mahakama kuwa ‘scupper’ hizo huwa zinafungwa wakati wa shughuli ya uchakataji samaki na kwamba kwa mazingira hayo ilionesha kuwa shughuli hiyo ilikuwa ikiendelea hata muda mfupi kabla ya kuwakamata.
Pia Jaji Mwarija alielezea kuridhika na ushahidi wa alama zilizooneshwa katika rada ya meli hiyo, ambazo zilionesha eneo walilokamatiwa baharini lilikuwa ni la Tanzania.
“Pia maelezo ya onyo ya washtakiwa wa 17 na wa 19 walikiri kuwa walipokamatwa walikuwa wakiendesha shughuli za uvuvi katika eneo la Tanzania,” alisema Jaji Mwarija na kuongeza;
“Kwa kuzingatia ushahidi huo, kosa la kuendesha shughuli za uvuvi katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania limethibitishwa,”alisema
Jaji Mwarija.
Maelezo mengine
Jaji huyo pia alisema anakubaliana na maoni ya Wazee Washauri wa Mahakama , Bernard Ntumba na Margreth Mosi kuwa washtakiwa wa kwanza na wa tisa wana hatia na wengine hawana hatia.
Kuhusu kutokuwa na leseni, Jaji Mwarija alisema ni jambo ambalo halikupingwa kuwa meli haikuwa nayo na kwamba mshatakiwa wa kwanza, (nahodha) alikubali na kisha akatoa nakala ya leseni ambayo ilikuwa imeisha muda wake.
Alisema kitendo cha mshtakiwa wa saba (wakala) kuja Dar es Salaam na kutoa nakala ya leseni kwa ofisa wa Polisi ambayo pia ilikuwa imekwisha muda wake, ni dhahiri kuwa naye alikuwa anawajibika kwa suala hilo.
“Hivyo, mshtakiwa wa kwanza na wa saba kwa pamoja wanatiwa hatiani kwa kosa hilo la kwanza,” alisema Jaji Mwarija.
Kuhusu kosa la pili la kuchafua mazingira ya bahari, Jaji Mwarija alisema kimantiki kushindwa kuleta uchafu yaani matumbo, mapezi na vichwa vya samaki mbali ya kilo tatu tu za utumbo ni dhahiri kuwa ulikuwa ukitupwa baharini.
Jaji Mwarija alisema jambo hilo halihitaji ushahidi wa kisayansi katika kulithibitisha, kama ambavyo upande wa utetezi ulivyodai wakati ukiwasilisha hoja zao za mwisho.
Kuhusu kosa la tatu la kusaidia kuwaepusha washtakiwa wengine na hatia lililokuwa likiwakabili mshtakiwa wa saba na wa tisa, Jaji Mwarija alisema kwa kuwa mshtakiwa wa saba ametiwani hatiani kwa kosa la kwanza hivyo, kosa la tatu hana hatia.
“Hivyo, mshtakiwa wa kwanza na wa saba wana hatia katika kosa la kwanza,” alisema Jaji Mwarija na kunyamaza kuwapa nafasi mawakili wa pande zote kusema lolote kabla ya kutamka adhabu.
Maelezo na hukumu
Wakili Mwandamizi wa Serikali Biswalo Muganga licha ya kukiri kuwa hawana kumbukumbu za washtakiwa hao waliotiwa hatiani kutenda makosa kama hayo, lakini aliiomba mahakama iwape adhabu kali.
Pia alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mambo ya Uvuvi na kwa mujibu wa kifungu cha 351 cha Kanuni za Adhabu, aliiomba mahakama iamuru meli hiyo iliyotumika kutenda makosa hayo itaifishwe baada ya washtakiwa kutiwa hatiani.
Hata hivyo, Kiongozi wa mawakili wa washtakiwa, nahodha Ibrahim Bendera aliyekuwa akisaidiana na John Mapinduzi aliiomba mahakama iwaonee huruma katika kutoa adhabu akidai kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kutenda kosa hilo kama alivyokiri wakili wa serikali.
Alidai washtakiwa hao wamekaa rumande kwa takribani miaka mitatu wakati kesi yao ikiendelea, hivyo kuiomba mahakama katika kutoa adhabu izingatie muda huo waliokaa rumande.
Alidai kuwa aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza (Nahodha) mwaka huu anatimiza miaka 63 na kwamba, miaka mitatu wameitumia rumande na kwa kuwa wana familia huko kwao.
Hata hivyo, aliishauri mahakama meli hiyo ifanyiwe tathmini ili ikiwezekama mwenye meli alipe fidia na kuchukua meli yake ili kuiondolea serikali mzigo wa kuikarabati.
Akitoa adhabu, Jaji Mwarija alisema amezingatia hoja za pande zote lakini akasema adhabu za makosa hayo zimeainishwa katika sheria ikiwa ni pamoja na kiwango cha chini ambacho mahakama haiwezi kukivuka.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Deep Sea, mahakama inaweza kutaifisha chombo kilichotumika kwenye uhalifu, hivyo meli hii ambayo ilikamatwa na kutolewa hapa kama kielelezo inataifishwa” alisema Jaji Mwarija.
Alisema uamuzi huo umezingatia mazingira kwamba ilifanya kazi kwa kutumia majina mengi tofauti na ilikuwa haitambuliki katika mamlaka inayosimamia Uvuvi wa Samaki aina ya Jodari katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.
“Mwenendo huo huonesha kuwa walifanya makosa hayo kwa mpango. Hivyo ili kuzuia uhalifu huu usiendelee kutokea mahakama imeamuru itaifishwe,” alisema Jaji Mwarija na kuongeza;
Kuhusu amri juu ya samaki waliopatikana kwenye meli, kwa sababu waligawiwa katika taasisi mbalimbali za kijamii, hakuna amri hoyote juu ya samaki hao, washtakiwa wana haki ya kukata rufaa.
Washtakiwa hao na wenzao walikamatwa Machi 8, 2009 wakiwa samaki tani 293 aina ya Jodari.
Awali, kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 37 wenye uraia wan chi tofauti wan chi za Bara la Asia na wawili walikuwa raia wa Kenya.
Julai 14, 2011 wengine waliachiwa huru baada ya kuoneakana kuwa hawana kesi ya kujibu isipokuwa washtakiwa watano ambao walihukumiwa jana na wawili kutiwa hatinai.
Hadi wakati hukumu yao inapotolewa washtakiwa hao wamesota rumande kwa miaka miwili, miezi 11 na siku 15.
MGAO WA UMEME WANZA KIMYA KIMYA
MAKALI ya mgao wa umeme, mkoani Mara yameanza kimya kimya na sasa unakatwa
kwa zaidi ya saa 10.Mpaka sasa wateja wa Tanesco, hawajatangaziwa nini
kinaendelea, licha ya uongozi wa shirika makao makuu kutoa taarifa tofauti.
Habari kutoka kwa ofisa mmoja wa shirika hilo alisema siyo mgao huo unatokana na kampuni inayozalisha umeme ya Aggreco kukosa mafuta ya kuendeshea mitambo yake.
Habari kutoka kwa ofisa mmoja wa shirika hilo alisema siyo mgao huo unatokana na kampuni inayozalisha umeme ya Aggreco kukosa mafuta ya kuendeshea mitambo yake.
“Kampuni hiyo inazalisha zaidi ya megawati 100 zinazoingizwa kwenye gridi ya
taifa, tumeambiwa haina mafuta tunatakiwa kupunguza watumiaji. Bunda, Serengeti
na Musoma wako kwenye mgao kuanzia saa 2:00 asubuhi mpaka saa 12:00 jioni na
hii itachukua muda.
Alisema Wilaya ya Serengeti, waliingia gizani tangu Februari 21 jioni mpaka Februari 22, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni uchakavu wa nguzo katika eneo la Bunda na Ushashi na kwamba tatizo hilo limekuwa likijirudia mara kwa mara mvua zinaponyesha.
Alisema Wilaya ya Serengeti, waliingia gizani tangu Februari 21 jioni mpaka Februari 22, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni uchakavu wa nguzo katika eneo la Bunda na Ushashi na kwamba tatizo hilo limekuwa likijirudia mara kwa mara mvua zinaponyesha.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Edward Ole Lenga alitoa tangazo wakati wa misa
ya Jumatano ya majivu katika kanisa katoliki Mugumu kuwapo kwa mgao huo.Baadhi
ya wananchi wameendelea kulalamikia uzembe wa Tanesco wa kutorekebisha nguzo
chakavu ambazo zinasababisha wakazi wa Serengeti kutokuwa na umeme.
Meneja wa Tanesco mkoa hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini mameneja wa wilaya walikiri kupokea ratiba za mgao wa umeme kwa mkoa huo.Maneja wa wilaya walisema tatizo la mgao linasababishwa na ukosefu wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya kampuni ya Aggreko.
Hali kama hiyo pia imeripotiwa katika mikoa ya Arusha na dodoma Meneja wa Tanesco mkoa hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini mameneja wa wilaya walikiri kupokea ratiba za mgao wa umeme kwa mkoa huo.Maneja wa wilaya walisema tatizo la mgao linasababishwa na ukosefu wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya kampuni ya Aggreko.
source:Mwananchi.


No comments:
Post a Comment